Baada ya kushindwa majaribio katika klabu inayoshiriki Ligi Kuu England ya West Ham, winga machachari wa Yanga, Mrisho Ngassa, imedaiwa kuwa wakala wake ana mpango wa kumrejesha nchini kwa lengo la kusajili timu ya Azam SC ambayo wakala huyo ni mmoja wa wakurugenzi wake.
Imedaiwa mchezaji huyo yupo njiani kujiunga na Azam, na kupelekwa kwake Uingereza ambapo ilionekana ni vigumu kushinda majaribio ilikuwa ni `janja` ya kuwazuga wana Yanga wasielewe kinachoendelea.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kwa mmoja wa wadau wa soka na mtu wa karibu wa mchezaji huyo (jina tunalo) ni kwamba Ngassa anafanyiwa mipango ya kutua Azam kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
“Huyu jamaa aliyempeleka Uingereza ni mmoja wa wakurugenzi wa Azam na hivyo katika kuzuga watu ameamua kumpeleka Uingereza ambapo anajua kwa vyovyote atafeli na kisha kuhamia timu yake ya Azam,“ amesema.
Hata hivyo, chanzo hicho kilipobanwa kina uhakika gani na jambo hilo, kikasema uhakika huo utabainika mara mchezaji huyo atakaporejea nchini.
“Kama huniamini, basi we subiri, Ngassa atajiunga na Azam tu, kwani mipango hiyo ipo siku nyingi tu,“ chanzo hicho kimesema.
Lakini Alasiri ilipowasiliana na wakala wake Yusuph Bakhresa, simu yake ilipokelewa na mtu aliyedai ni msaidizi wake na kusema habari hizo ni za uzushi.
“Hivi huko Bongo hamna la kufanya, yaani hata kabla majibu yake (Ngassa) ya kufaulu au kufeli hayajatolewa, tayari mmeshazua mengine kuwa anaenda Azam, kakuambia nani?“ msaidizi huyo ambaye hata hivyo jina lake halikufahamika mara moja alihoji.
Awali Bakhresa alisema iwapo winga huyo atashindwa majaribio West Ham atafanyiwa mipango ya kufanya majaribio mengine, Fulham ambayo pia inashiriki Ligi Kuu.
- SOURCE: Alasiri