Menu
in , , , ,

AZAM IMEFUNGWA NA SIMBA INAYOJITAFUTA

Tanzania Sports

Jana kwenye uwanja wa New Amani Complex kulichezwa derby ya Mzizima. Derby ambayo ilikuwa na ushindani ndani na nje ya uwanja lakini mwisho wa siku Simba SC ilifanikiwa kushinda dhidi ya Azam FC ambaye ni mwenyeji wa mchezo huo.Zifuatazo ni sababu tano ambazo zilichangia ushindi wa Simba SC dhidi ya Azam FC.

ENEO LA KIUNGO CHA AZAM FC

Kwenye mechi ya jana eneo la kiungo cha Azam FC wakicheza James Akaminko, Adolf Mtesigwa pamoja na Feisal Salum maarufu kwa jina la “Fei Toto”. James Akaminko na Adolf Mtesigwa walikuwa wanacheza katika mstari mmoja wa chini. Wote kwa pamoja muda wote walikuwa eneo la chini ya kiungo na kuwe na uwazi kati ya eneo la kiungo cha kuzuia na eneo la kiungo cha kushambulia.

Hali hii ilikuwa inamfanya Feisal Salum kushuka chini kufuata mpira, kila alipokuwa anashuka eneo la chini ya kiungo kulikuwa kunafanya eneo la mbele kuwe na uwazi pia hivo hata huduma za mpira kwenye eneo la mbele ilikuwa hafifu. Pia kitendo cha Feisal kushuka chini kufuata mpira kulikuwa kunapunguza idadi ya watu eneo la mbele hivo kumfanya Saidun kubaki pekee yake bila huduma nyingi.

WASHAMBULIAJI WA PEMBENI WA AZAM FC

Baada eneo la kiungo cha kati cha Azam FC kutotoa huduma nyingi kwenye safu ya ushambuliaj, eneo pekee lililokuwa linatazamiwa ni eneo la pembeni ambapo walicheza Nado pamoja na Gibril Silla. Wote wawili walikuwa wanakaa pembeni sana ya uwanja kitu ambacho kilikuwa kinapunguza idadi ya watu kwenye box la Simba SC na kujikuta Simba SC wapo wengi eneo lao. Pia wote wawili hawakutengeneza nafasi jana.

UDHAIFU WA  BEKI WAO YORO

Mara nyingi Yoro alikuwa na makosa mengi binafsi jana. Nyakati nyingi hakuwa eneo lake sahihi mfano goli la kwanza la Simba SC alilofunga Lionel Ateba lilifungwa Yoro akiwa hayupo kwenye eneo lake sahihi. Pia jana Azam FC walikuwa wanacheza kwa kuanza mashambulizi kwa nyuma. Ili uweze kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma lazima mabeki wawe na uwezo wa kupiga pasi kitu ambacho hakikuwepo kwa Yoro.

MFUMO MZIMA WA KUJILINDA WA SIMBA SC

Moja ya kitu ambacho Simba SC imefanikiwa mpaka muda huu ni namna ambavyo wanajilinda kwa pamoja. Simba SC haitoi nafasi kwa mpinzani kupata nafasi kwenye eneo lao ndiyo maana jana Azam FC walifanikiwa kupata shot on target moja tu. Simba SC ilikuwa inatoa nafasi kwa Azam FC kumiliki mpira kwenye nusu yao Azam FC lakini kila walipokuwa wanafika nusu ya Simba SC hakukuwepo na nafasi ya wao kufunga.

Jana Azam FC imefungwa na Simba SC inayojitafuta kwa sababu maeneo mengi Simba SC haijakamilika vyema eneo peke yake ambalo Simba SC inaonekana kucheza vyema ni eneo la kujilinda.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Leave a Reply

Exit mobile version