*Ni wazi kuwa mwalimu Arsene Wenger hakutaka kutawala mchezo huo*
Arsenal waliwafunga Manchester United kwa mabao matatu kwa sifuri jana Jumapili. Ingawa walifungwa lakini Manchester United walitawala sehemu kubwa ya mchezo huo kwa umiliki wa mpira, idadi ya pasi na hata usahihi wa pasi.
Ukizitazama takwimu za Arsenal za umiliki wa mpira na idadi ya pasi zilikvyokuwa kabla ya mchezo wa juzi dhidi ya United utagundua kuwa Arsene Wenger aliamua kubadili mbinu na mikakati yake kwa ajili ya kukabiliana na Manchester United ambao kabla ya mchezo huo walikuwa vinara wa EPL.
Kabla ya mchezo dhidi ya United Arsenal walikuwa wanaongoza kwa wastani wa umiliki wa mpira wakiwa na takribani asilimia 60. Mchezo pekee wa EPL ambao Arsenal walizidiwa kwa umiliki wa mpira ni mchezo dhidi ya Chelsea na nafikiri kadi mbili nyekundu walizoonyeshwa Gabriel Paulista na Santi Cazorla zilichangia.
Kwenye mchezo wa ufunguzi ambao walifungwa 2-0 dhidi ya West Ham, Arsenal walikuwa na umiliki wa mpira wa asilimia 62 West Ham wakiwa na 38. Mchezo wa pili dhidi ya Crystal Palace uliwashuhudia Arsenal wakiwa na umiliki wa mpira wa asilimia 59.
Katika michezo mitatu iliyofuatia dhidi ya Liverpool, Newcastle na Stoke City takwimu za Arsenal kwenye umiliki wa mpira ziliendelea kuwa nzito ambapo walikuwa na ziadi ya asilimia 65 kwenye kila mchezo kati ya hiyo mitatu. Kwenye mchezo uliofuatia dhidi ya Chelsea ndipo kadi nyekundu zilipowafanya wazidiwe kwene umiliki wa mpira kabla ya kutawala tena kwa asilimia 58 dhidi ya Leicester.
Manchester United wao kabla ya mchezo wa juzi walikuwa na wastani wa umiliki wa mpira wa asilimia 57 ambazo ni chache ukilinganisha na zile 60 za Arsenal kabla ya mchezo huo.
Kutokana na takwimu hizo wengi tulitarajia kuwaona Arsenal wakitawala kwenye umiliki wa mpira kwenye mchezo wa juzi dhidi ya Manchester United lakini hilo halikuweza kutokea. Washika bunduki hao wa London walimiliki mpira kwa asilimia 38 pekee huku United wakitawala kwa asilimia 62.
Hata ukitazama idadi ya pasi zilizopigwa kwenye mchezo huo Arsenal waliachwa mbali na Manchester United. United walipiga pasi 651 wakati Arsenal walipiga 403. Hili pia halikutarajiwa kwa kuwa kabla ya mchezo huo Arsenal walikuwa na wastani mkubwa wa idadi ya pasi kuwazidi Manchester United.
Ni wazi kuwa mwalimu Arsene Wenger hakutaka kutawala mchezo huo. Alibadili mbinu na kuamua kulinda zaidi na kutafuta mianya ya kufanya mashambulizi ya kustukiza. Hili liliwezekana kutokana na kasi ya wachezaji wa Arsenal hasa Theo Walcott aliyepiga pasi mbili za mabao.
Pia Francis Coquelin na Santi Cazorla walifanya kazi nzuri mno kwenye kuzima mashambulizi ya wapinzani na kuwasambazia mipira washambuliaji wao mara moja. Mianya ya kusambaza mipira hiyo ilikuwa wazi mno kwa kuwa United walifunguka zaidi wakijaribu kusawazisha mabao mawili ya mapema yaliyofungwa dakika ya 6 na ya 7.
Hali ilizidi kuwa mbaya zaidi kwa upande wa Manchester United waliporuhusu bao la tatu kwenye dakika ya 19. Wakafunguka zaidi na Arsenal wakarudi nyuma kulinda. Mara nyingi wachezaji 9 mbaka 10 walikuwa nyuma ya mpira wakishiriki kwenye kulinda mabao hayo.
Muda mrefu mpira ulichezwa kwenye upande wa Arsenal lakini bado Arsenal hao hao waliongoza kwa idadi ya mashuti. Walipiga mashuti 12 huku Manchester United wakipiga 9. Hivyo ndivyo namna Wenger alivyofanikiwa kuwachapa United 3-0 kwa kubadili mbinu zake.