RAIS mpya wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Evans Aveva, amesema kwamba anawaahidi wanachama wa klabu hiyo waliomchagua hatawaangusha baada ya kumpa ridhaa ya kuwaongoza katika kipindi kingine cha miaka minne atakayokaa madarakani kwa mujibu wa katiba.
Aveva alifanikiwa kuibuka mshindi katika uchaguzi huo ambao awali ulizingirwa na ‘mizengwe’ mbalimbali hadi kufikia kusimamishwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakati wa mchakato wake kwa kupata kura 1,455 dhidi ya mpinzani wake aliyekuwa anaungwa ‘mkono’ na wafuasi wa Michael Wambura, aliyeenguliwa, Andrew Tupa, aliyepata kura 388.
Akizungumza muda mfupi baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi hiyo katika uchaguzi uliofanyika juzi Jumapili kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi Oysterbay jijini, Aveva, alisema kuwa anafahamu kazi yake anayotakiwa kuifanya akiwa madarakani ambayo wanachama wa Simba imewaumiza kwa kipindi cha miaka minne iliyomalizika.
Aveva alisema kwamba atahakikisha anavunja makundi yaliyopo katika klabu hiyo ili kuleta umoja, ushirikiano na mshikamano ndani ya klabu hiyo na anafahamu wazi makundi hayo yalikuwepo kama sehemu ya kutekeleza demokrasia ya kila mwanachama.
Alisema kuwa makundi hayo yatakapomalizika ndipo mafanikio na maendeleo ya pamoja yatatimia na hilo ndiyo jambo ambao Wana-Simba wanatakiwa kulitekeleza kwa pamoja ili kufikia malengo waliyojiwekea.
“Nina kazi kubwa mbele yenu, naamini sitowaangusha, nitafanya kazi kwa umakini mkubwa ili kufikia malengo tuliyojiwekea, nawashukuru wote walioniunga mkono na hata wale ambao hawakunipigia kura kwa sababu kila mmoja ametumia haki yake ya kidemokrasia, nawapongeza pia wagombea wengine walioshinda na wale waliokosa kura zao hazikupotea ila ni maamuzi ya wanachama yanatakiwa kuheshimiwa,” alisema Aveva.
Aliongeza kuwa uchaguzi umemalizika na kinachotakiwa kufuata ni wanachama kujipanga kwa ajili ya kuimarisha umoja na utulivu ili mpira uchezwe ndani ya timu yao.
AHADI ALIZOTOA
Wakati aliposimama kuomba kura kwenye ukumbi huo wa uchaguzi, Aveva, alisema kuwa mara atakapofanikiwa kuingia madarakani atahakikisha anaongeza idadi ya wanachama wa klabu hiyo kutoka 7,000 na kufikia 50,000.
Aveva alisema kuwa anaamini kwa kuongeza wanachama, klabu yao itaweza kupata rasilimali watu na kujiweka katika nafasi nzuri ya kujiongezea mapato na kuwataka wanachama wawe wanalipa ada zao kila mwaka na si kusubiri wakati wa uchaguzi.
Alisema anauzoefu ndani ya Simba na akiwa mwenyekiti wa kamati mbalimbali alizoziongoza aliipatia klabu mafanikio hivyo watarajie mazuri zaidi baada ya yeye kupata ridhaa ya wanachama ya kuwa rais mpya na wa kwanza wa Wekundu wa Msimbazi.
WENGINE WALIOSHINDA
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo saa 9:58 usiku wa kuamkia jana Jumatatu, Mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi na aliyesimamia zoezi hilo, Amin Bakhresa, alisema kuwa mshindi wa nafasi ya Makamu wa Rais ni Geofrey Nyange ‘Kaburu’ ndiye aliibuka kidedea kwa kupata kura 1,046 na kuwashinda Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ (412), Swedy Mkwabi (373) na Bundala Kabula aliyeambulia kura 25.
Bakhersa pia aliwatangaza wagombea watano waliochaguliwa kuunda Kamati ya Utendaji kuwa ni pamoja na zilichukuliwa na Iddi Kajuna aliyepata kura 893, Said Tully (788), Collins Frisch (758), Ally Suru ( 627) na kwa upande wa mwanamke aliyeibuka kinara ni Jasmine Badour
.
Mjumbe huyo wa kwanza mwanamke kuingia katika uongozi alipata kura 933 na kuwagalagaza wapinzani wake Asha Muhaji aliyepata kura 623 na Amina Poyo (330).