Macho yangu yalikuwa yanaitazama Arsenal. Najua kulikuwa na mechi nyingi sana ambazo zilikuwa zinachezwa tena ambazo zilikuwa na ushindani mkubwa sana. Unaweza ukajiuliza kwanini sikutaka kuitazama mechi ya Leicester City na Manchester United?
Mechi ambayo ilikuwa inaamua ni timu ipi ambayo ingepata nafasi ya kushiriki ligi ya mabingwa barani ulaya. Mechi ambayo wengi waliitengenezea mazingira kuwa itakuwa mechi ya ushindani kulingana na timu zote kuwa na hitaji linalofanana ( kushiriki ligi ya mabingwa barani ulaya msimu ujao).
Inawezekana pia ukajiuliza kwanini sikutaka kuitazama mechi ya Aston Villa? Mechi ambayo ilikuwa imebeba maamuzi kama Mtanzania mwenzetu Mbwana Ally Samatta atabaki ligi kuu ya England au atashuka daraja? Najua ungejiuliza sana bila kupata majibu kwanini mechi ya Arsenal na Watford ndiyo ilikuwa mechi yangu mwishoni mwa juma hili.
Jibu sahihi la kwanini mimi niliamua kuchagua mechi hii ni Pierre -Emerick Aubameyang. Hii ndiyo sababu ya kwanini mimi niliamua kuchagua mechi hii , siyo kwamba Pierre Emerick Aubameyang ni mchezaji bora sana na wa kuvutia sana kutazamwa kuzidi wote kwenye ligi kuu ya England, La hasha! Ila nilitaka kuutazama uso wa Pierre Emerick Aubameyang.
Mboni za macho yangu zilikuwa na shauku kubwa sana kumuona Pierre- Emerick Aubameyang kwenye mechi ambayo haikuwa na faida kwa Arsenal. Arsenal hata angeshinda goli 10 asingekuwa na uwezo wa kuingia angalau hata kwenye nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi kuu ya England.
Nilitaka kutazama uso wa Pierre- Emerick Aubameyang ukizungumza nini kwenye mechi ya mwisho katika ligi. Nilitamani kufahamu kama uso wake ulikuwa unazungumza hatima yake katika timu ya Arsenal msimu ujao ?
Arsenal hatoshiriki tena ligi ya mabingwa barani Ulaya na kuna uwezekano wa wao kutoshiriki michuano ya Uefa Europa League kama hawatofanikiwa kubeba kikombe cha FA. Swali kubwa ambalo lilikuwa kichwani kwangu ni Pierre Aubameyang atakubali kuendelea kucheza kwenye timu ambayo haina nafasi kubwa kwenye michuano ya ulaya msimu ujao?
Uso wake ulikuwa unazungumza nini? Alikuwa anaaga rasmi au alikuwa anaonesha kuwa hata msimu ujao ataendelea kuwepo ndani ya kikosi cha Arsenal ? Macho yangu yalibahatika kumuona akifunga goli mbili , kila alipokuwa akifunga goli nilikuwa namtazama vizuri usoni mwake, lengo langu ni kufahamu kuwa ana furaha ndani ya Arsenal au hana furaha?
Ilikuwa ngumu sana kung’anus hiki kitu kwa sababu muda wote Pierre Aubameyang anapofunga huwa anatabasamu. Huwa anafurahia kufunga, furaha yake kubwa kwenye maisha ni kufunga magoli. Hapa ndipo niliposhindwa kuelewa haswa maana halisi ya kicheko cha Pierre Emerick Aubameyang.
Sikutaka kufikiria sana kuhusu hatima yake ndani ya Arsenal kama ataondoka au atabaki. Binafsi mimi napenda aendelee kubaki kwa sababu ligi kuu ya England , ligi pendwa inayofuatiliwa na watu wengi inahitaji kuwa na wachezaji wenye ushindani mkubwa kama yeye , anahitajika sana kwenye ligi hii pendwa.
Kama anahitajika kuna kitu ambacho Arsenal wanatakiwa kumtengenezea. Wanatakiwa kumtengenezea mazingira ya yeye angalau kuwa mchezaji wa kuacha alama ndani ya klabu ya Arsenal.
Kuna wachezaji wengi washawahi kuacha alama ndani ya klabu ya Arsenal kama kina Henry, Van Persie, Drake , Brain n.k . Wachezaji hawa walitengenezewa mazingira ya wao kuacha alama . Moja ya mazingira ambayo yalitengenezwa ni wao kuwa na watu bora ambao waliwazunguka.
Wetu ambao walikuwa na uwezo wa kutengeneza nafasi kwa ajili yao, watu ambao walikuwa na uwezo wa kutengeneza mazingira ambayo yangewafanya wao wang’are Pierre Aubameyang amekuja katika kipindi kigumu sana. Kipindi ambacho hakuna aina ya viungo wa kati wanaotengeneza nafasi nyingi za magoli.
Kipindi ambacho hakuna wachezaji wa mbele ambao ni wabunifu kwa kiasi kikubwa. Kwa bahati mbaya zaidi amekuja kwenye kipindi ambacho Mesut Ozil ashazeeka , macho yake yamepoteza mwangaza , login yake imepoteza uwezo wa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga kama mwanzo. Zawadi pekee ambayo Pierre Aubameyang anatakiwa kupatiwa na Arsenal ni kuletewa kiungo ambaye ana sifa kama Mesut Ozil wa kipindi kile yuko kijana.