*Newcastle na Spurs wapeta 16 bora
*Chelsea waponea, Liverpool watoka
Atletico Madrid wametema ubingwa wa Europa League licha ya ushindi bao 1-0 dhidi ya Rubin Kazan wa Urusi.
Mshambuliaji anayewaniwa na klabu kubwa za Ulaya, Radamel Falcao alifunga bao pekee la mechi ya Alhamisi kwa timu hiyo ya Hispania, lakini wakafungishwa virago kwa wastani wa mabao 2-1.
Waliharibu mambo wenyewe wiki moja kabla nyumbani kwao, walipokubali kichapo cha mabao 2-0.
Atletico walipambana kulinda heshima yao, wakaelekeza mashuti 18 langoni mwa wapinzani wao lakini moja tu likazaa tunda ambalo halikutosha.
Katika mechi nyingine, Tottenham Hotspurs walijihakikishia wanaingia hatua ya 16 bora, baada ya bao la Moussa Dembele katika dakika ya 90 ya mchezo.
Hadi wakati huo, Lyon walikuwa wakiongoza kwa bao 1-0, hivyo kufanya wastani wa mabao kuwa 2-2, kutokana na matokeo ya wiki iliyotangulia nchini England.
Spurs walionekana kutokuwa makini kipindi cha kwanza, hali iliyotumiwa na wapinzani wao vyema kupata bao, lakini wageni walizinduka nusu ya pili, na kufanikiwa mwishoni.
Kwa ushindi huo, Spurs watamenyana na Inter Milan ya Italia waliowatandika Cluj wa Romania kwa jumla ya mabao 5-0.
Newcastle waliokwenda suluhu nyumbani na Metalist Kharkiv, wamefanikiwa kuwafunga wapinzani wao hao bao moja nyumbani kwao Ukraine na kuvuka hatua hii ya timu 32.
Ilikuwa ni penati ya Shola Ameobi iliyowavusha vijana hao wa Allan Pardew, katika mechi ambayo
Papiss Cisse alikosa nafasi mbili za wazi kuiweka mbele timu yake.
Newcastle walipata penati baada ya Moussa Sissoko kuangushwa na golikipa Olexandr Goryainov kwenye eneo lake la kujidai.
Chelsea nao wamevuka kwa bahati ya bao la dakika ya 90 lililofungwa na Eden Hazard dhidi ya Sparta Prague na mechi kumalizika kwa bao 1-1.
Hata hivyo, Chelsea wanavuka kwa jumla ya mabao mawili, kwani katika mechi ya kwanza nchini Czech Chelsea walishinda kwa bao 1-0. Sparta walilinda bao walilopata dakika ya 17, lakini Chelsea wakawazidi pumzi, labda na bahati na kuwatoa.
Liverpool walirekebisha makosa ya mchezo wa kwanza kwa kuwashinda Zenit St Petersburg mabao 3-1, lakini Warusi wamevuka kwa kanuni ya bao la ugenini.
Katika mechi ya kwanza nchini Urusi, Zenit waliwatambia Liverpool kwa mabao 2-0, hivyo Liverpool walihitaji ushindi wa mabao 3-0 au 4-1, lakini hawakumudu.
Liverpool walianza vibaya mechi ya Alhamisi hii kwa kufungwa bao dakika ya 19, kabla ya Joe Allen kufunga moja na Luis Suarez mawili, lakini bado hayakutosha.
FC Basle kutoka Uswisi nao wamefuzu kwa wastani wa mabao 3-1 dhidi ya Dnipro Dnipropetrovsk wa Ukraine.
Timu nyingine iliyofuzu ni Lazio wa Italia waliowashinda Borussia Moenchengladbach kutoka Ujerumani kwa jumla ya mabao 5-3. Stuttgart nao wamevuka kwa kuwaelemea Genk 3-1.