Atletico Madrid wamefuta uteja kwa klabu mbili kubwa za Real Madrid na Barcelona kwa kutwaa ubingwa wa nchi.
Atletico wanaofundishwa na Diego Simeone walitwaa ubingwa kwa staili ya aina yake, kwani waliwavua mabingwa watetezi, Barcelona.
Zaidi ya hapo, waliwatoa nishai kwa kuwalazimisha sare ya 1-1 kwenye mechi ya mwisho ya msimu na kuipata pointi moja tu waliyokuwa wakihitaji.
Barca walikuwa wanahitaji pointi tatu ili kutetea ubingwa wao lakini licha ya kuwa na wachezaji maarufu duniani hawakufurukuta.
Kutokana na hali hiyo, Kocha wa Barcelona, Gerardo Martino ‘Tata’ ameamua kuachia ngazi na kuwaomba radhi washabiki kwa kushindwa kutimiza ndoto yao.
Tata alichukua nafasi hiyo kwa mkataba wa miaka miwili lakini ameondoka kabla hata ya kufikia nusu, akiwa amerithi nafasi ya hayati Tito Vilanova aliyejiuzulu kwa sababu ya maradhi ya saratani ya shingo.
Atletico wamefikisha pointi 90 na kuwaacha Barca na Real wakiwa na pointi 87 kila moja. Atletico watakipiga tena wikiendi ijayo na Real Madrid katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika hatua nyingine, Juventus wa Italia wameweka rekodi mpya katika ligi 10 bora barani kwa kufikisha pointi 102.
Juve wamemaliza ligi kwa kuwa mabingwa wakiwa na pointi 17 zaidi ya Roma walioshika nafasi ya pili. Juve wameshinda mechi zao zote 19 za nyumbani.