Menu
in ,

Athari ya uamuzi wa Robin van Persie kwa Arsenal

NA: Israel Saria
————–
Uamuzi wa Robin van Persie kutosaini mkataba mpya una athari kubwa kwa majaliwa ya Arsenal kama klabu.
Imeshabainika kwamba nahodha huyo wa Washika Bunduki wa London ameng’aka kutoa saini mkataba mpya, akisema kuna kutofautiana kifalsafa na viongozi kuhusu mipango ya baadaye ya klabu hiyo.
Van Persie anakuja baada ya mlolongo wa wachezaji nyota wengine kutaka kuondoka Arsenal. Msururu huo wa wachezaji mahiri kutaka kuondoka dimba la Emirates unajenga picha tofauti na jinsi Arsenal inavyochukuliwa kwa ujumla kama klabu ya hadhi ya juu kabisa.

Aleksandr Hleb, Emmanuel Adebayor, Cesc Fabregas, Samir Nasri na sasa van Persie walianza shinikizo la kutaka kuondoka tangu msimu wa 2007/08.
Wachezaji hawa walikuwa wakitafuta kipato kikubwa zaidi, lakini pia wakataja ukweli wa kuwa na kiu ya kupata nafasi kwenye klabu yenye matumaini zaidi ya kushinda taji.
Iwe kauli za aina hii zinaaminiwa kwa namna tu zinavyotolewa au la, ukweli ni kwamba hadhi ya Arsenal kwenye soka inatibuliwa kila mara mchezaji nyota anapobwaga manyanga na kutafuta klabu nzuri zaidi.
Kwa kadiri athari zinavyozidi kuongezeka na kutokezea kila mara, hatari inayoinyemelea Arsenal si nyingine zaidi ya ile ya kuwa klabu ya kuuza wachezaji muhimu kila wakati.
Madhali wachezaji muhimu wanaendelea kuondoka kwa sababu ya klabu kuonekana haina malengo ya dhati, basi Arsenal itaanza kuonekana kama eneo la kuzalisha wachezaji kwa ajili ya klabu kama Manchester City na Barcelona.
Kukua kwa dhana hiyo kunawachochea washabiki na wadau wa Arsenal ambao tayari wamezongwa na machungu na hamu ya kupata kombe, baada ya kupitisha misimu saba bila chochote kwenye mashindano ya ndani na kimataifa.
Ikishafika kiwango hicho cha kukosekana utulivu na matumaini, basi ni wazi shinikizo litapindukia upande wa pili wa Bodi ya Arsenal, ili wakae na kubadili sera zao za fedha.
Sera ya mapato na matumizi inayoonekana kila wakati kutekelezwa na kutolewa mfano na Kocha Mkuu, Arsene Wenger inachukuliwa kama msingi mkuu wa madhila yanayoiandama klabu sasa na sababu ya wachezaji wengi nyota kuamua kuikimbia.
Kwa hiyo basi, hata siku BBC.co.uk itakaporipoti kwamba Manchester United inaingia kwenye Soko la Hisa la New York kwa ajili ya kupata suluhu ya madeni yake, Arsenal watabaki kuelekezewa chagizo badala ya kupongezwa kwa jinsi wanavyobana matumizi.
Kuondoka kwa Robin van Persie, ama msimu huu wa kiangazi au ule ujao, litakuwa pigo jingine kubwa zaidi kwa Arsenal, timu yenye msingi wa wachezaji chipukizi, lakini inayopata ufufutende katika kutumia fedha ili kujiweka juu kama klabu kwenye soka ya kisasa.
saria@tanzaniasports.com

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version