Kocha mpya wa Aston Villa, Tim Sherwood ameendelea vyema na kazi yake jijini Birmingham baada ya vijana wake kuingia nusu fainali ya michuano ya Kombe la FA.
Sherwood aliyefukuzwa Tottenham Hotspur bila sababu za kuridisha, amewasaidia Villa kufika hatua hiyo ya juu kwa mara ya kwanza tangu 2000 walipotinga Wembley.
Villa wamewafunga wagumu West Bromwich Albion ambao pia wanaye kocha mpya katika Tonny Pulis anaejulikana kwa mbinu za kuzuia vigogo na pia kuokoa timu kwenye hali mbaya.
Huu pia ni ushindi wa pili kwa Mwingereza Sherwood ndani ya wiki moja dhidi ya wapinzani hao ambao wote wanatoka eneo la kati ya nchi.
Katika mechi iliyogubikwa na washabiki kuonesha utovu wa nidhamu, walikuwa Villa walioondoka na ushindi muhimu kwa mabao ya kipindi cha pili ya Fabian Delph na Scott Sinclair.
Hali ya hewa ilizidi kuchafuka uwanjani hapo baada ya mchezaji wa West Brom, Claudio Yacob alipopewa kadi nyekundu baada ya kuwa amelambwa ya pili ya njano, na washabiki wa timu yake kuzidi kuchukizwa.
Baadhi ya washabiki wa West Brom, klabu maarufu kwa jina la Baggies, walifikia hatua ya kung’oa viti majukwaani na kuvitupa uwanjani. Washabiki wa Villa walivamia dimbani kushangilia kabla mwamuzi Anthony Taylor hajapuliza kipenga cha kumaliza mechi.
Wakati Taylor akihitimisha mechi, washabiki wengi wa Villa waliingia uwanjani, huku mchezaji wa Baggies aliyetokea benchi, Callum McManaman alijaribu kukabiliana nao kwa hasira kabla ya kuchukuliwa kupelekwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Villa hawajapata kufunga bao katika mechi tano za nusu fainali zilizopita ambazo walibahatika kushiriki, hivyo ni wakati wa Sherwood kuonesha kwamba wanaweza.
Villa nao walimaliza mechi wakiwa na wachezaji 10, kwani mchezaji wao Jack Greallish naye alipewa kadi ya pili ya njano na hatimaye nyekundu kwa mchezo mbaya.