Nahodha wa Timu ya Taifa ya Ghana na mchezaji wa zamani wa Sunderland, Asamoah Gyan amekanusha kuhusika na kifo cha mwanamuziki wa miondoko ya kufoka foka, Castro.
Pamekuwa na tetesi za mshambuliaji huyo kuhusika na kuwazamisha Castro na mpenzi wake, Janet Badu, walipokuwa wote wakila raha. Gyan alialika rafiki zake kadhaa kutembelea klabu yake ya starehe iitwayo Aqua Safari Resort iliyopo kusini mwa nchi ndipo maafa yakatokea.
Polisi walikuwa wakiendelea kutafuta miili ya wawili hao, na sasa watu wameeneza uvumi ndani na nje ya Ghana kwamba mwili wa Castro ulitumiwa kama kafara maalumu ya uganga ili Gyan apate utajiri.
Gyan – mchezaji anayeshikilia historia ya kufunga mabao mengi zaidi katika Timu ya Taifa ya Ghana ‘Black Stars’ kwa sasa anachezea klabu ya Al Ain ya Emarati baada ya kusajiliwa mwaka 2011 kwa mkopo akitoka Wearside.
Waliokuwa kwenye kundi la maraha na Gyan ni Emmanuel Tagoe a.k.a Game Boy na dada yake, Naa; Theophilus Tagoe; Castro; Alberta Tetteh aliyefika na rafiki zake wa kike, Nana Akua Ayisi and Janet Bandu; Benjamin Owusu Ansah; Dauda Tetteh; Patrick Botchway; Akwasi Bonsu; Kwabena Boateng;Joseph Kissi; Seth Tetteh; DJ George na mwanasheria Kissi Agyabeng.
Gyan aliitisha mkutano na waandishi wa habari ambapo mwanasheria huyo Agyabeng alisema safari hiyo ilikuwa ya kawaida tu. Julai 5 mwaka huu kundi hilo lilihamia kwenye klabu nyingine iliyo jirani – Peace Holiday Resort ambapo Castro na Gyan akashiriki kwa furaha.
Hata hivyo, kesho yake, Castro na Janet waliamua kwenda na boti kufurahia maisha lakini hawakurudi hadi leo. Inaelezwa kwamba Gyan aliwahi kupata ajali ya boti akiwa na Castro, na wanaoamini uchawi wanasema zilikuwa njama za Gyan kumteketeza.
Gyan pia amempoteza mama yake mzazi hivi karibuni, kifo kilichofuatiwa na cha rafiki yake wa karibu, ambaye watu wengine wanadhani walikuwa na urafiki wa mashaka. Mwanasheria huyo alisema ingetarajiwa watu wamliwaze Gyan, lakini wamemgeuza kuwa muuaji.