Mikel Arteta ametangazwa kuwa nahodha mpya wa Arsenal, baada ya Thomas Vermaelen aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo kuhamia Barcelona.
Kocha Arsene Wenger ametangaza kwamba Arteta (32) aliyesajiliwa kwa pauni milioni 10 kutoka Everton mwaka 2011 anachukua nafasi hiyo rasmi baada ya Arsenal kuwalaza Manchester City 3-0 na kutwaa Ngao ya Jamii Jumapili hii.
Beki wa kati wa Arsenal, Per Mertesacker ametajwa kuwa nahodha msaidizi kuanzia hiyo jana. Mjerumani huyo bado yupo kwenye mapumziko baada ya kushiriki kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil.
Akizungumza Jumapili, Arteta ambaye anacheza nafasi ya kiungo, amesema taji hilo walilopata ndani ya siku 85 baada ya lile la Kombe la FA ni muhimu kwao, kwa sababu walikaa muda mrefu bila kombe lolote.
Raia huyo wa Hispania aliyekuwa nahodha msaidizi, amesema ilikuwa vyema kujipima kwenye mechi ya Jumapili kujua walipo kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuu na kwamba kuna maeneo waliyothibitisha ni wazuri.
Arteta amesema kwamba walikabiliana na mabingwa wa England na kufanikiwa kuwalaza, baada ya kutofanya vyema walipokabiliana na timu kubwa mwishoni mwa msimu uliopita. Akasema Jumapili ilikuwa fursa ya kusawazisha mambo, na wameonesha kwamba wanaweza na wamerejesha kujiamini kwao.
Arteta amesema kwamba anaamini wapo kwenye mwelekeo sahihi kutokana na usajili uliofanywa, lakini pia jinsi wenzake wanavyojituma na kwamba hana wasiwasi wa kupata ushirikiano wao, kwani msimu uliopita alivaa mara nyingi beji ya nahodha wakati Vermaelen akiwa benchi.