Menu
in , , ,

Arsenal wawachapa Man City

*Liverpool wabaki kujiuliza kulikoni

Arsenal wamepunguza pengo dhidi ya vinara wa ligi Leicester, kwa
kuwachapa Manchester City 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya England
(EPL).

Wakicheza nyumbani Emirates, Arsenal walionesha dhamira ya kutaka
kuliendea taji ambalo hawajalipata tangu 2004, wakicheza vyema na
kuonesha nidhamu uwanjani, ambapo hakuna mchezaji wao aliyeoneshwa
kadi yoyote.

Man City walitawala mchezo kwa asilimia 63 lakini Arsenal walimudu
kuwazuia hadi dakika ya 82 Yaya Toure alipofunga bao la kufutia
machozi, huku ya Arsenal yakifungwa na Theo Walcott kutoka umbali wa
yadi 20 na Olivier Giroud.

Kiungo wa Arsenal, Mesut Ozi aliendelea kutoa pasi za kuzaa mabao na
sasa amefikisha 15, mara mbili zaidi ya mchezaji mwingine yeyote
katika EPL. Kevin de Bruyne wa wa City alionesha udhaifu kwa kushindwa
kutumia fursa ya kufunga wakati beki wao, Eliaquim Mangala aliboronga
kwenye ulinzi.

City walionekana kuamka dakika za mwisho lakini Toure na Wilfried Bony
walipoteza nafasi nzuri za kusawazisha bao, huku Arsenal wakiwabana
hadi dakika ya mwisho kujihakikishia pointi tatu muhimu.

Washika Bunduki wa London pamoja na kufunga, walikuwa wazuri kwenye
ulinzi, wakiwa na mabeki wao waliofanya kazi ya ziada, Nacho Monreal
na Per Mertesacker, huku golikipa Petr Cech akionesha kwamba Arsene
Wenger hakukosea kumsajili.

Arsenal watacheza na Southampton ugenini Desemba 26 kabla ya kupambana
na Bournemouth nyumbani siku mbili baadaye. Manchester City watakuwa
nyumbani kucheza na Sunderland kabla ya kukwaana na vinara Leicester
Desemba 28.

Kwa ushindi huo, Arsenal wamefikisha pointi 36, mbili nyuma ya
Leicester na nne zaidi ya Man City. Tottenham wanashika nafasi ya nne
wakiwa na pointi 29 sawa na Man United na Crystal Palace.

LIVERPOOL WANA MASWALI YA KUJIBU

Mamadou Sakho na Lucas, walionekana wachezaji wa kawaida sana...
Mamadou Sakho na Lucas, walionekana wachezaji wa kawaida sana…

Liverpool wanaendelea kujiuliza kilichowafanya wakapoteza mechi na
pointi muhimu Jumapili, pale walipochabangwa na Watford 3-0 katika
dimba la Vicarage Road.

Liverpool walianza vibaya mechi hiyo na kuadhibiwa mapema kwa mabao ya
Nathan Ake baada ya kona ya kwanza iliyochongwa na Adam Bogdan dakika
ya tatu tu ya mchezo.

Mnigeria Odion Ighalo aliwaliza tena Liverpool dakika chache baada ya
hapo kisha Mnigeria huyo akapigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la
vijana wa Jurgen Klopp akipokea vyema majalo ya Valon Behrami.

Watford ndio kwanza wamepanda daraja lakini kwenye msimamo wa ligi
wapo vizuri katika eneo ambalo wakiendelea hivyo wanaweza hata kucheza
Ligi ya Mabingwa Ulaya, kwani wapo nafasi ya saba wakiwa na pointi 28.
Huo ulikuwa ushindi wao wa nne mfululizo.

Kichapo kinawaacha Liverpool wakiwa hawajapata ushindi wowote katika
mechi tatu za EPL zilizopita na wanabaki nafasi ya tisa, zikiwa ni nne
nyuma ya Watford wanaofundishwa na Quique Flores, aliyesema ushindi
uliwafurahisha sana.

Klopp alisema kwamba Liverpool wanatakiwa kubadili ‘kila kitu’,
akiongeza kwamba kuna kitu hakikwenda sawa na anatakiwa afikirie tena
kwa sababu ni makosa na atajifunza kutokana nayo.

Katika mechi nyingine, Swansea walikwenda suluhu na West Ham. Swansea
hawana kocha baada ya kuondoka kwa Garry Monk, lakini wameonekana kuwa
wazuri kuliko awali walipokuwa wakipoteza mechi mfululizo.

Wanabaki katika eneo la kushuka daraja kwa pointi zao 15 wakifuatiwa
na Sunderland wenye 12 na mkiani kabisa wapo Aston Villa ambao wana
pointi saba.

Timu zote hizi zimebadili makocha, ambapo Sunderland wanaye Sam
Allerdyice baada ya Dick Advocaat kuondoka mambo yalipozidi kuwa
magumu wakati Villa wamemchukua Remi Garde, mchezaji wa zamani wa
Arsenal.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version