*Man U, Chelsea waweka rekodi EPL
Arsenal wamefanikiwa kuvuka mechi za mchujo na kuingia moja kwa moja kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), baada ya kuwatoa Fenerbahce.
Arsenal waliwakaribisha Waturuki hao katika dimba la Emirates jijini London, wakiwa na faida ya mabao 3-0 waliyofunga nchini mwao.
Shujaa wa Arsenal usiku wa Jumanne hii alikuwa Aaron Ramsey aliyepachka bao la kwanza katika dakika ya 25 kufuatia pasi nzuri ya Mjerumani Lukas Podolski.
Kiungo huyo wa Wales alicheka tena na nyavu kuandika bao la pili katika dakika ya 72 baada ya kupatiwa mpira na beki wa kushoto Kieran Gibbs.
Kwa ushindi huo, Arsenal wanavuka hatua za mtoano kwa jumla la mabao 5-0.
REKODI MECHI MAN UNITED NA CHELSEA
Katika mechi ya Ligi Kuu usiku wa Jumatatu, Manchester United walitoka suluhu na Chelsea katika dimba la Old Trafford.
Hiyo ilikuwa mechi kubwa na ya kwanza kuwakutanisha makocha wapya wa klabu hizo mbili, David Moyes wa Man U na Jose Mourinho wa Chelsea.
Kadhalika imeweka rekodi ya suluhu, kwa sababu tangu 2009 Manchester United hawakupata kutoa sare ya bila kufungana na timu yoyote hapo katika mechi za ligi.
Moyes alieleza kusikitishwa kwake na sare hiyo tasa, akalalamika kunyimwa penati baada ya mpira kumgonga Frank Lampard mkononi na Chelsea wakalalamika kunyimwa nyingine baada ya Ashley Cole kuanguka au kuangushwa ndani ya 18.
Wayne Rooney aliyekuwa akitarajiwa kuhamia Chelsea alicheza vyema kwa kila namna, lakini tu hakuweza kufunga bao, huku Mourinho akipanga kikosi kisichotarajiwa, akimwacha benchi Juan Mata na hakuanzisha mshambuliaji yeyote rasmi ambaye ni mpachika mabao.