*Everton safi, wengine waambulia sare
Kama ulikuwa unawatilia shaka Arsenal, basi huna budi kuendelea kuwasubiri hadi kipenga cha mwisho, kwani mauaji yao hayana mpaka.
Wakicheza nyumbani Emirates katika mechi muhimu, walijikuta wamepokea kichapo cha bao moja hadi dakika ya 84 kutoka kwa Norwich City.
Vijana wa Arsene Wenger hawakukata tamaa, bali waliweka shinikizo katika lango la wapinzani wao na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 85 kwa penati ya Mikel Arteta, baada ya Olivier Giroud kuchezewa vibaya.
Goli hilo liliwapandisha mzuka The Gunners, ambao dakika tatu baadaye walifanya kweli kwa Giroud kucheka na nyavu baada ya kutengewa na Alex Oxlade-Chamberlain.
Mjerumani Lukas Podolski aliyeingia dakika ya 59 badala ya Yao Gervinho aliachia fataki lililozaa bao la mwisho dakika ya 90.
Bao la Norwich lilifungwa na Michael Turner kwa kichwa, kutokana na mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Robert Snodgrass.
Kwa ushindi huo, Arsenal wamesogea nafasi ya tatu kwa kujikusanyia pointi 59, wakati Norwich wanaingia katika majaribu ya kushuka daraja, kwani wapo nafasi ya 14 kwa pointi 35, pointi nne tu kutoka eneo la hatari.
Arsenal wamefanikiwa kuwapita mahasimu wao wa London Kaskazini, Tottenham Hotspurs kwa pointi moja, na wanawapita Chelsea kwa pointi hiyo pia, lakini Chelsea wana mchezo mmoja mkononi.
EVERTON WAENDELEA KUPAMBANA
Everton wameendeleza kampeni yao kuwania nafasi ya uwakilishi Ulaya, baada ya kuwafunga Queen Park Rangers 2-0 na kufikisha pointi 55.
Toffees, kama wanavyojulikana Everton walifunga kupitia Darron Gibson dakika ya 40 na Vctor Anichebe dakika ya 56.
Hayo yalikuwa maumivu makubwa kwa QPR ya Harry Redknapp, kwani wamesogezwa zaidi kwenye ukingo wa kushuka daraja, hasa baada ya kupoteza ushindi wa dhahiri kwenye mechi iliyopita dhidi ya Wigan.
QPR wanabaki nafasi ya pili kutoka mwisho kwenye msimamo wa ligi, wakiwa na pointi 24, wakati Everton wanaofundishwa na David Moyes wanashika nafasi ya sita, nyuma ya Spurs.
ASTON VILLA BADO WAPO HATARINI
Aston Villa wamelazimishwa sare na Fulham, hivyo kupunguza kasi yao ya kuondoka kwenye maeneo ya hatari ya kushuka daraja.
Timu zote zilipoteza nafasi nyingi za kufunga, kabla ya Charles N’Zogbia kuzifumania nyavu dakika ya 56. Jitihada hizo zilifutwa na mchezaji mwenzake, Fabian Delph aliyejifunga dakika ya 66 akitaka kuokoa kona ya Bryan Ruiz.
Sare hiyo inawaacha Fulham bila matatizo, kwani wana pointi 40 wakiwa nafasi ya 10, lakini kocha wao, Martin Jol alikuwa anasema ana hamu ya ushindi walau mmoja kwenye mechi zilizobaki.
SAINTS, WEST HAM ZAJIIMARISHA
Sare baina ya Southampton na West Ham United imekuwa ya faida kwa timu zote, zikielekea kujihakikishia kubaki ligi kuu msimu ujao.
West Ham walipigana kiume kupata sare hiyo nyumbani kwa Saints, ambapo Gaston Ramirez alitangulia kuwainua washabiki wa nyumbani kwa bao safi dakika ya 59.
Mchezaji wa Liverpool anayecheza West Ham, Andy Carroll alidhihirisha umuhimu wa mkopo wake huko, baada ya kusawazisha bao dakika ya 66 kwa mpira wa adhabu ndogo alioupiga chini chini.
Timu zote mbili zimefikisha pointi 38, Southampton wakiwa nafasi ya 11 kwa uwiano wa mabao -7 wakifuatiwa na West Ham wenye uwiano wa mabao -9.
READING WAAMBULIA SULUHU
Reading wanaoaminika kuwa katika safari ya kushuka daraja, wameambulia suluhu mikononi mwa Liverpool.
Ilikuwa pointi ya kwanza kwa kocha mpya Nigel Adkins ambaye kabla ya kuingia Reading alifukuzwa Southampton, lakini bado wanashika mkia kwenye msimamo wa ligi.
Hayakuwa matokeo mazuri kwa Liverpool wanaotafuta nafasi ya kucheza Ulaya, na watajilaumu kwa kushindwa kutumia nafasi nyingi walizopata.
Golikipa wa Reading, Alex McCarthy alitokea kuwa mchezaji bora wa mechi na shujaa kwa timu yake, baada ya kuokoa zaidi ya michomo 10 iliyokuwa ikielekewa wavuni.
Shuti la mfungaji anayeongoza kwenye ligi, Luis Suarez liliokolewa kwenye mstari wa goli, ambapo teknolojia mpya ingekuwa inatumika si ajabu lingehesabiwa kuwa bao.
Suluhu hiyo inawaacha Liverpool nafasi ya saba wakiwa na pointi 50, wakihitaji pointi nane ili kupanda kwenye eneo la kuingia Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku wakiombea walio juu wafungwe mizunguko watakayoshinda wao.
Manchester City wapo nafasi ya pili kwa pointi zao 65 huku mahasimu na jirani zao, Manchester United wakiwa nafasi ya kwanza kwa pointi 77.
WIGAN FAINALI KOMBE LA FA
Wigan wanaochechemea kwenye Ligi Kuu, wamefanikiwa kuingia fainali ya Kombe la FA, baada ya kuwafunga Milwall mabao 2-0 uwanjani Wembley.
Wigan wanaoshika nafasi ya 18 kwenye msimamo wa ligi, waliingia uwanjani kwa kishindo, wakiongozwa na Mwenyekiti Dave Whelan na kocha Roberto Martinez, wakiweka historia hata kama watashuka daraja.
Bao la kwanza la Wigan lilifungwa na Shaun Maloney dakika ya 25 akiwa ndani ya boksi la penati, baada ya kupokea pasi ya Arouna Kone.
Wigan walijihakikishia ushindi kwa bao la pili la Callum McManaman katika dakika ya 77 aliyepewa pasi na Jordi Gomez. Wigan watacheza fainali na ama Chelsea au Manchester City uwanjani hapo hapo Mei 11 mwaka huu.