Menu
in , , ,

Arsenal warudia nafasi ‘yao’

*Reading na QPR kisicho riziki hakiliki

*Liverpool waamka na kufanya mauaji

Arsenal walioahidi kurejesha makali wiki iliyopita, wamerejea kwenye eneo la nafasi nne za juu walizozoea.

Ushindi wao dhidi ya Wigan, japo mwembamba wa bao 1-0 na kushindwa kwa Tottenham Hotspur kuwafunga Stoke, kumewapaisha Arsenal.

Bao la penati la mtaalamu wao wa siku hizi, Mikel Arteta katika dakika ya 60 limetosha kuwafikisha nafasi ya tatu.

Hapo ni nyuma ya mahasimu majirani wa Manchester, yaani Manchester United wenye pointi 42 na Manchester City waliojikusanyia 39. Arsenal wana 30.

Hata hivyo, Chelsea wapo nyuma kwa michezo miwili na hata wakitoka sare tu wataichukua nafasi ya tatu, kwani sasa wana pointi 29 na walikuwa Japan kwenye michezo ya kombe la klabu la dunia.

Huu ni ushindi wa tatu mfululizo wa Arsenal tangu Machi mwaka huu, lakini Wigan watajilaumu kwa kukosa mabao, hasa kupitia mshambuliaji Arouna Kone ambaye ama alikosa shabaha au kipa Wojciech Szczesny. Wigan wanashika nafasi ya 18 kati ya timu 20 zinazoshiriki ligi kuu hii.

Arteta alifunga penati baada ya mshambuliaji wa kati, Theo Walcott kuchezewa rafu alipokuwa akijiandaa kufunga. Bado Walcott anajivuta katika kukubali mkataba mpya klabuni hapo, tofauti na wengine watano waliosaini hivi karibuni.

Kocha Arsene Wenger alitania kwa kusema kwamba sasa Arsenal wameondoka kwenye kile alichokiita ‘mgogoro mkubwa’, tangu walipoanza kujinasua huko kwa kuwachabanga Reading mabao 5-2 Jumatatu iliyopita.

Everton wameendelea kukabana koo na Arsenal, baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya West Ham United. Wamefikisha pointi 30, lakini Arsenal wanawazidi kwa uwiano mzuri wa mabao.

West Ham walitangulia kufunga bao kupitia kwa Carlton Cole aliyetolewa kwa kadi nyekundu iliyolalamikiwa sana, kwa madai alimchezea rafu Leighton Baines.

Spurs wanaofundishwa na Andre Villas-Boas walikuwa na nafasi nzuri ya kula bata Krimasi hii kwa furaha zaidi wakiwa nafasi ya tatu au ya nne, lakini walishindwa.

Wakicheza nyumbani White Hart Lane, Spurs walishindwa kufungua vyumba vya wagumu Stoke City, hivyo kuambulia suluhu.

Stoke hawajafungwa katika mechi nane mfululizo sasa, lakini wamekuwa vijana wa kuizoea sare. Tottenham wanabaki nafasi ya tano kwa sasa.

Reading wanaokalia chini ya msimamo wa ligi wameendelea kupoteza mechi katika mazingira ya kutatanisha, safari hii ikiwa ni dhidi ya mabingwa wa England, Manchester City.

Pamoja na ukubwa wa jina, City hawakufurukuta kwa dakika 91 dimbani mbele ya Reading, lakini dakika ya 92 ilishuhudia Gareth Barry akiwafungia City bao tata.

Kocha wa Reading, Brian McDermott alisema walisikitishwa na kushangazwa na uamuzi wa refarii, na kwamba baada ya safari ndefu na mchezo safi, haki yao ilikuwa walau pointi moja kwa suluhu.

Bale anaonekana alifunga bao hilo baada au wakati akifanya rafu, lakini ndio hivyo limeshawapatia City pointi tatu muhimu za kufukuzana na United.

Bale aliweka mikono yake juu ya Nicky Shorey wa Reading ili kupachika bao kutokana na majalo ya mwenzake, David Silva.

Reading wanalia pia kwamba walistahili penati, baada ya mchezaji wao Jay Tabb kuangushwa chini na beki wa kushoto wa City, mwenye umri wa miaka 18, Karim Rekik aliyecheza mara ya kwanza Jumamosi hii.

Ama upande mwingine, Newcastle wamejaribu kufuta machungu ya kufungwa mabao 3-1 na City wiki iliyopita, kwa kuwafunga kwa tabu Queen Park Rangers bao 1-0.

Hicho ni kipigo cha kwanza kwa QPR chini ya kocha mpya, Harry Redknapp, kikija baada tu ya ushindi wao wa kwanza baada ya mechi 16 za kufungwa na sare.

Newcastle walicheza nyumbani St James’ Park, lakini walionekana kuchoka, wakiwa wamepoteza mechi sita zilizopita. Demba Ba na Papiss Cisse walikosa mabao, hadi Shola Amoebi alipokuja kufunga dakika 10 za mwisho.

Vijana wa Anfield, Liverpool wamepata ushindi wao mkubwa zaidi wa msimu, walipowakung’uta Fulham mabao 4-0.

Wakicheza chini ya Brendan Rodgers, Liverpool walifunga mabao yao kupitia kwa Martin Skrtel, nahodha Steven Gerrard , Stewart Downing na Luis Suarez.

Kwa ushindi huo, Liverpool waliopoteza mechi iliyopita, sasa wanashika nafasi ya nane wakiwa na pointi 25. Fulham wapo nafasi ya 13 kwa pointi zao 20.

West Bromwich Albion walioanza ligi vizuri kabla ya kupepesuka kwa wiki kadhaa zilizopita, wamefanikiwa kupata ushindi Jumamosi hii.

West Brom walimaliza jeuri ya Norwich ya kutofungwa katika michezo 10 na kutamba kwa kufunga vigogo, kwa kuwafunga mabao 2-1.

Kocha wa West Brom, Steve Clark anasema katika ligi hii, ukicheza mechi nyingi bila ushindi, unaweza kuzoea na likawa tatizo kubwa.

Kwamba walitaka kumaliza tatizo hilo kabla ya sikukuu ya Krismasi, na kweli wamepata ushindi siku tatu kabla.

West Brom sasa wanashika nafasi ya sita wakiwa na pointi 30 wakati Norwich ni wa 10 kwa pointi zao 25.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version