*Wawafyatua Norwich 4-1
*Manchester United sare
Vinara wa Ligi Kuu ya England, Arsenal wameendelea kujikita hapo baada ya ushindi mnono dhidi ya Norwich.
Wakicheza katika dimba la Emirates, Arsenal walipata mabao yao kupitia kwa viungo Jack Wilshere, Aaron Ramsey na Mesut Ozil aliyefunga mawili.
Norwich walipata bao lao kupitia kwa Jonny Howson, ambapo vijana hao wa Carrow Road walionesha kuwa tishio katika baadhi ya nyakati, lakini Arsenal walifanikiwa kumaliza mechi ya 12 bila kupoteza.
Katika mechi nyingine, mabingwa watetezi, Manchester United waliendelea kudorora baada ya kutoka sare ya 1-1 na Southampton.
Ilikuwa alasiri chungu kwa kocha David Moyes ambaye bado hajaweza kuwaweka vizuri United, ambapo Robin van Persie alifunga bao la kuongoza lakini Saints wakasawazisha dakika moja kabla ya kipenga cha mwisho kupitia kwa nahodha wao, Adam Lalana.
Hali hiyo inawaacha United wakijiuliza iwapo wataweza kutetea ubingwa wao, kwa sababu wamebaki pointi nane nyuma ya vinara wa ligi hiyo.
Manchester City kwa upande mwingine waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya West Ham, wakipata mabao yao kupitia kwa Sergio Aguero aliyefunga mawili na David Silva wakati West Ham walifungiwa na Vaz Te.
Huu ulikuwa ushindi wa kwanza kwa City ugenini msimu huu na kuwa furaha kubwa kwa kocha Manuel Pellegrini.
Liverpool waliporeza kasi yao baada ya kwenda sare ya mabao 2-2 na Newcastle, Chelsea wakawafunga Cardiff 4-1 katika mechi ambayo kocha Jose Mourinho alipewa kadi nyekundu kwa utovu wa nidhamu.
Everton walirejea kwenye hali nzuri kwa kuwafunga Hull 2-1, Swansea wakawakung’uta Sunderland 4-0 na Stoke wakaenda suluhu na West Bromwich Albion.
Kwa hali hiyo, Arsenal wanaongoza wakiwa na pointi 19 wakifuatiwa na Chelsea na Liverpool zenye pointi 17 kila moja.
Man City wanafuata kwa pointi zao 16, Southampton wana 15 sawa na Everton, wakifuatiwa na Tottenham Hotspur katika nafasi ya saba huku Man United wakijiburuza kwenye nafasi ya nane.
Sunderland wamebaki mkiani wakiwa na pointi moja baada ya mechi nane, wakati wa pili kutoka chini ni Crystal Palace wenye pointi tatu na Norwich wana pointi saba.