Menu
in , ,

Arsenal waogelea kwenye fedha

*Arsenal wametakata kifedha, ambapo wametangaza faida ya pauni milioni 17.8

 

Ukwasi huo unawapa matumaini wadau kwamba kocha Arsene Wenger atabadilika na kununua wachezaji nyota wa kimataifa kuimarisha kikosi chao.

Washabiki wanaomlalamikia Wenger kwa mkono wake wa birika wakati wa usajili unapowadia, wanafurahia tangazo la klabu yao kupata faida hiyo kwa nusu mwaka.

Wakati akaunti za klabu zikinona na wenye mali kufaidi, dimbani timu inaonekana kuendelea kuwa dhaifu mwaka hadi mwaka, ambapo huu ni mwaka wa nane bila kutwaa taji lolote.

Awali kisingizio kilikuwa kipaumbele cha kujenga uwanja, lakini sasa Emirates imekamilika na mikataba mikubwa ya kibiashara imetiwa saini, hivyo hakuna sababu ya kutopigana vikumbo na klabu nyingine kubwa kwenye usajili.

Pamoja na mapato mengine, mwishoni mwa msimu uliopita Arsenal walimuuza mchezaji bora wa mwaka, mpachika mabao wao bora na nahodha, Robin van Persie kwa Manchester United kwa pauni milioni 24.

Hazina ya Washika Bunduki hao wa London sasa inafikia pauni milioni 123.3 taslimu, ambapo washabiki wake, Arsenal Supporters’ Trust (AST) wanasema kuna haja ya kiasi kikubwa zaidi kutengwa kwa ajili ya timu.

Msemaji wa AST anasema inashangaza Arsenal kuendelea kutengeneza faida kwa kuuza wachezaji wake bora, lakini akasema washabiki wamechangia kwa kulipa tiketi ambazo ni kati ya ghali zaidi duniani.

Mwenyekiti wa Arsenal, Peter Hill-Wood anasisitiza kwamba uthabiti huo wa kifedha ndio msingi wa timu kuwa kwenye nne bora na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Pictured: Kieran Gibbs, Jack Wilshere, Aaron R...
Pictured: Kieran Gibbs, Jack Wilshere, Aaron Ramsey, Vito Mannone (Photo credit: Wikipedia)

“Shabaha yetu ni kuona kila mdau anajivunia klabu hii. Tunajua hiyo yaweza kuwa kwa kutwaa mataji, lakini pia kwa jinsi tunavyofanya mambo yetu na kubaki imara,” akasema mwenyekiti huyo.

Washabiki wanaamini kwamba bado mapengo yaliyoachwa na wachezaji kama Van Persie, Samir Nasri na Cesc Fabregas hayajazibwa. Hill-Wood anasema wana lengo la kuhakikisha wachezaji nyota wanabaki na kusajili wengine wenye vipaji kuiimarisha timu.

Mwenyekiti anasema licha ya kusikitishwa kuondoka RVP, wachezaji wao wazuri wameongeza mikataba ya muda mrefu, nao ni Jack Wilshere, Theo Walcott, Kieran Gibbs, Aaron Ramsey, Alex Oxlade-Chamberlain na Carl Jenkinson.

Kadhalika walinunua wachezaji wa kimataifa, Lukas Podolski, Santi Cazorla na Olivier Giroud na Januari akaongezwa Nacho Monreal.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version