Menu
in , , , ,

Arsenal wanaweza kurudi Ligi ya Mabingwa Ulaya

Tanzania Sports

Pépé was a treat to watch

Ni hakika macho ya wapenzi ya soka yana shauku kubwa kuona urejeo wa Arsenal kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL)tena, kwani ni takribani msimu wa tatu mfululizo sasa wanashindwa kushiriki ligi hiyo, wakiishia kushiriki Ligi ya Europa.

Mara ya mwisho Arsenal kushiriki mashindano hayo makubwa zaidi Ulaya kwa ngazi ya klabu walipoteza bao 5-1 nyumbani dhidi ya Bavarians – Bayern Munich ndio ulikuwa usiku wa mwisho wa wapenzi wa soka kuona Washika Bunduki wa London wakiacha alama ndani ya UCL.

Msimu uliofuata ‘babu’ Arsene Wenger aliwaongoza Arsenal kutinga hatua ya nusu fainali ya Europa lakini wakashindwa kutinga fainali baada ya kutupwa nje na Atletico Madrid, msimu ukaisha na Wenger baada ya miaka yake zaidi ya 20 ndani ya EPL akabwaga manyanga.

Ilikuwa furaha iliyoje kwa washabiki wa Arsenal walioanza kushika mabango zaidi ya miaka sita nyuma wakitaka aondoke; mzee aliyedumu Arsenal tangu 1996, wakati huo Arsenal wakiwa chini ya Mwenyekiti Peter Hill-Wood aliyemwamini na kumng’oa huko Nagoya Grampus Eight ya nchini Japan. Kweli hakuna mwanzo usio kuwa na mwisho.

Wakati baadhi ya nchi zikitambua umri wa mtu mzima ukianzia miaka 18, basi Wenger aliishi Arsenal kwa zaidi ya miaka miwili ya mtu mzima na kufikia ukomo mwaka 2018. Wakati akiondoka zake, katika nchi aliyozaliwa kwenye viunga vya Le Parc Des Princes; maskani kwa Paris Saint-Germain (PSG) nako Mhispania Unai Emery alifutwa kazi baada ya kushindwa kufikia matwaka ya matajiri hao wa Ufaransa.

Na ule msemo usemao ‘ukisema cha nini mwenzako anawaza atakipata lini’ ukatimia Arsenal wakampa kibarua Emery wakiwa na imani yale aliyoyafanya akiwa na Sevilla basi yatahamia Arsenal na kuendeleza mpira wa kuvutia na wenye kasi ndani ya Emirates. Kama ilivo ada kwa mwalimu mpya anapoanza kazi sehemu mpya, basi huleta wachezaji watakaomsaidia kupandikiza mbinu zake katika timu.

Ikamlazimu kumvuta Denis Suarez kwa mkopo kutoka FC Barcelona, akamnasa Stephan Lichtsteneir bure , akalipa pauni 17.6 kumnasa Sokratis Papastathopouls kutoka Borrusia Dortmund, akavunja kibubu tena kwa Sampdoria kumnasa kiungo Lucas Torreira. Hiyo haikutosha; akaenda Bayern Leverkusen akamvuta mlinda mlango Bernd Leno kwa ada ya uhamisho wa pauni 19.2 millioni, huku usajili ulioenda kimya kimya na kuja kuwaduwaza wengi ulikuwa baada ya kutoa pauni 7 miliioni kwa Lorient ili kupata huduma ya Mateo Guendouzi.

Licha ya kuanza kwa kusuasua, Emery alifanikiwa kushika nafasi ya tano katika ligi nyuma ya Manchester City ,Liverpool, Chelsea na Tottenham Hotspur waliomaliza ndani ya nne bora na kupata tiketi ya kushiriki UCL. Yote tisa pia ndani ya msimu huo Emeryi aliwaongoza Arsenal kutinga hatua ya fainali ya Europa huku macho na masikio ya wapenda soka hasa wapenzi wa klabu hiyo yakisubiri kuona wanarejea katika michuano yenye mvuto kwa ngazi za klabu duniani lakini waliduwazwa na Chelsea baada ya kubugizwa mabao 4-1 na kujikuta wanakosa nafasi ya kurudi UCL.

Wakati shauku na matamanio ya mashabiki wa Arsenal ni kuona timu yao inarrejea katika ushiriki wa UCL, mmoja ya wawekezaji katika klabu hiyo Stan Kroenke pamoja na bodi nzima iliwalazimu kutoa zaidi ya pauni miliioni 100 kwa ajili ya msimu huu kuhakikisha wanafanya vizuri katika ligi ili wapate nafasi ya kushiriki ligi ya mabingwa barani ulaya. Fedha hizo Wenger angezitumia kwa misimu minne lakini wao wakatumia katika majira ya kiangazi kuwanasa nyota kama Nicolas Pepe ,Wiliiam Saliba,Kieran Tierney ,David Luiz na Gabriel Martinelli.

Licha ya matumizi ya fedha nyingi katika usajili hiyo haikumaanisha ndio kufanya vizuri katika ligi; Emery aliwaongoza Arsenal katika michezo 78 katika mashindano yote akishinda 43 na kupoteza 19 na akitoa sare michezo 16. Hakika mwenendo huo haukuwaridhisha mabosi wa Arsenal na ikawalazimu kumfuta kazi Emery na kumpa timu Freddie Ljungberg kwa muda kabla ya kumpa mikoba mchezaji wao wa zamani Mikael Arteta.

Licha ya kukabidhiwa mikoba Arteta hajafanikiwa sana kuwarejesha Arsenal katika makali yaliozoewa, labda kwa kuwa amepokea kijiti njiani na kwa hali jinsi ilivyo Arsenal msimu ujao huenda wakakosa tena ushiriki wa UCL huku msimamo mpaka sasa ukionesha wakiwa nafasi ya 10 na alama zao 34 wakizidiwa alama saba na Chelsea wanaoshika nafasi ya nne.

Wamefikia hapo baada ya mechi 26, wakiwa na tofauti ya uwiano wa mabao mawili nan i baada ya kuwagaragaza Newcastle kwa mabao 4-0 Jumapili hii kwenye dimba la Emirates. Walianza mechi kwa kubanwa na Newcastle wanaofundishwa na Steve Bruce.

Hata hivyo baada ya mazungumzo wakati wa mapumziko, walikianza kipindi cha pili na kuweka mabao na kuwarejeshea washabiki wao matumaini kwani ilikuwa nadra kupata ushindi, achilia mbali mkubwa kama huo, kwani walizoea sare. Yalikuwa mabao yaliyotokana na washambuliaji na viungo waliocheza kwa pamoja vyema kuanzia dakika ya 54.

Nahodha wao, Pierre-Emerick Aubameyang alirejea kwenye kufunga kama ilivyokuwa kwa Pepe, Ozil na Alexandre Lacazette ambaye kwa muda sasa amekuwa akiteseka kwa kushindwa kufunga. Arteta alieleza raha yake kwa Mfaransa huyo kurudi kuzifumania nyavu.

Licha ya wakongwe mbalimbali kukosoa mwenendo wa Arsenal wakidai wamepoteza hadhi lakini kwa upande wake Arteta anaeleza kwamba bado kikosi wana nafasi ya kurejea na kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya misimu iyayo

Anasema kwamba nafasi yao kushiriki UCL inabaki kwao kuwekeza nguvu kubwa na kuwa na mwanzo mzuri pindi ligi ya msimu ujao itakapoanza na hiyo itafufua matumaini na utawala mpya wa kurudi katika UCL

Aidha Arteta anahitaji kufanya mabadiliko baadhi ya maeneo katika kikosi chake hasa katika eneo la ulinzi kutokana na makosa ambayo yamekuwa yakitokea ni yale yale hasa kwa walinzi wake wa kati yaani Luiz na Sokrats. Hiyo inatokana na kucheza mechi nyingi bila kupumzika na kukosa mbadala sahihi.

Pia katika eneo hilo la ulinzi la Arsenal wanakosa kiongozi sahihi mwenye roho ya ‘kikatili’ atakayewamezesha ‘sumu’ walinzi wengine kuchukua uamuzi mgumu pindi inapohitajika. Mfano mzurini Liverpool wenye Virgil Van Djik; walinzi wenzake wanafuraha kucheza pamoja na wanamuona kama kiongozi ndani ya uwanja.

Hata hivyo, walinzi wa pembeni wa Arsenal si wapikaji wa mabao kama timu zinazofanya vizuri; ukiwatazama Liverpool wana Trent Alexandre-Arnold na Andrew Robertson wenye uwezo wa kutengeneza zaidi ya mabaoi 20 ( kwa pamoja ). Ni faida iliyoje, basi Arteta asajili mabeki wa pembeni wenye uwezo wa kupika mabao pindi timu inapocheza kwa kushambulia toka pembeni au kushambulia toka maeneo yote ya uwanja.

Pia eneo la kiungo cha ushambuliaji haishangazi kutofautisha uwezo wa Mesut Ozil yule wa Real Madrid na wa sasa kutokana na uwezo wake wa kupika mabao zaidi ya 15 ndani ya msimu mmoja kutoonekan tena. Itamlazimu Arteta kuvunja benki atafute kiungo mshambuliaji atakaye kuwa akifanya muunganiko mzuri toka kwa viungo wa chini yaani Granit Xhaka na Lucas Torreira na kuhakikisha washambuliaji Lazazette na Aubameyang wanafunga vya kutosha kutokana na nafasi zinazopatikana.

Eneo jingine ambalo Arteta anapaswa kuingia sokoni ni kusaka winga wa kushoto. Sina shaka na uwezo wa Pepe kwani siku za karibuni ameonesha ana kitu, hasa akipata watu sahihi wanaomzunguka, lakini upande mmoja hautoshi kuhakikisha Arsenal wanatisha hasa katika EPL na UCL. Ndiyo maana Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp anaweka meno yake 32 nje akiwa na Sadio Mane na Mohamed Salah ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa mhimili wa timu kwa misimu kadhaa.

Dunia inahitaji kuona Arteta akiacha alama katika soka na ndiyo maana hata bilionea Kroenke na Bodi ya Arsenal walikmuiba mikononi mwa Pep Guardiola wa Man City. Mzee aliyemleta Arteta Emirates yupo kapumzika anakutazama, ila akumbuke kwamba hata Roma haikujengwa kwa siku moja.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version