*Liverpool wamuwinda beki wa Chile
*Man United wamtaka Sami Khedira
Baada ya mfululizo wa wachezaji wake kuondoka kila mwaka, Arsenal wanajaribu kuvuna kwa wapinzani wao wa London, Chelsea.
Arsene Wenger amenukuliwa akisema anataka kumsajili beki kisiki wa Stamford Bridge, Branislav Ivanovic.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Serbia anatakiwa Emirates, katika hali ya kushangaza kidogo, ambapo Arsenal wanakadiria ada ya uhamisho inaweza kuwa pauni milioni saba.
Kiasi hicho cha fedha kinaweza kumshawishi kocha Jose Mourinho kumuuza Ivanovic (30) ili pia kuwianisha vyema hesabu za klabu au kununua beki mwingine mdogo.
Habari hizo zinakuja wakati nyingine zikisema kwamba Wenger anataka kupata beki mwingine wa kati kabla ya kumruhusu nahodha Thomas Vermaelen kuondoka.
Anatajwa kutakiwa na Manchester United lakini mwenyewe akiwa Brazil na Timu ya Taifa ya Ubelgiji hakukana wala kukubalia, akidai yatasemwa mengi ila anaipigania nchi yake.
Hatima ya Ivanovic kikosini Chelsea ina kiwingu kutokana na uwapo wa Gary Cahill na John Terry kupewa kipaumbele huku Kurt Zouma anayeibukia akimpendeza zaidi Mourinho.
LIVERPOOL WAMUWINDA BEKI WA CHILE
Liverpool wamevutiwa na uchezaji wa beki wa Timu ya Taifa ya Chile, Mauricio Isla na wanataka kumsajili.
Kocha Brendan Rodgers anataka Isla anayechezea Juventus ili awe mbadala wa Glen Johnson ambaye katika miezi ya karibuni ameshuka kiwango.
Hata hivyo, alipoulizwa hivi karibuni, Isla alisema kazi yake ni Juve na Chile tu, anajua washabiki wanampenda na kwamba kocha ndiye atakuwa na uamuzi wa mwisho.
MANCHESTER UNITED WAMTAKA KHEDIRA
Wakati kocha mpya wa Manchester United, Louis van Gaal anadaiwa kuulalamikia uongozi wa klabu hiyo kwa kimya kinachotanda juu ya usajili, inaelezwa anamtaka Sami Khedira.
Man U wanamfuatilia Mjerumani huyo anayekipiga Real Madrid baada ya kusikia kwamba mabingwa hao wa Ulaya wanataka kumuuza.
Khedira (27) anachukuliwa kama mmoja wa viungo wanaoweza kumiliki mpira vyema zaidi Ulaya.
Huyu atakuwa mzuri kwenye mfumo anaoupenda Van Gaal wa 4-3-3, lakini Man U itabidi wajikung’ute pauni milioni 20. Inatambulika kwamba Arsenal na Chelsea wanamtaka pia.
Pamekuwa na habari kwamba Van Gaal atapewa pauni milioni 200 za usajili lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika wala fedha hazijatolewa kwa yakini.
LESCOT AJIUNGA WEST BROMWICH
Beki wa kati wa Manchester United aliyemaliza mkataba wake msimu huu, Joleon Lescot amejiuga na West Bromwich Albion.
Lescott alitafutwa na Aston Villa tangu Januari mwaka huu lakini amewapa mgongo na kwenda West Brom ambao nusura washuke daraja msimu huu.
Lescot (31) anakuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na kocha mpya, Alan Irvine na amepewa mkataba wa miaka miwili na ni hapo alipoanza kucheza kwenye akademia yao.
Mwingereza huyo amesoma shule moja – Four Dwellings Academy iliyopo Birmingham na Daniel Sturridge wa Liverpool. Alikuwa shabiki mkubwa wa Villa, na kocha Paul Lambert alikuwa anatumia kigezo hicho kumnasa.