Menu
in , , ,

ARSENAL WAKAMILISHA USAJILI WA LACAZETTE KWA ADA YA REKODI

Tanzania Sports

Alexandre Lacazette amejiunga rasmi na Arsenal kwa ada ya uhamisho ya paundi milioni 46.5 akitokea Lyon ya Ufaransa. Mshambuliaji huyo aliyekipiga katika Ligi Kuu ya Ufaransa kwa misimu kadhaa amesaini mkataba wa miaka mitano utakaomuweka jijini London mbaka majira ya joto ya mwaka 2022. Dau la paundi milioni 46.5 linamfanya kuwa mchezaji ghali zaidi kuwahi kusajiliwa na Arsenal akivunja rekodi ya Mesuit Ozil aliyejiunga na Washika Bunduki hao wa London mwaka 2013 akitokea Real Madrid kwa apaundi milioni 42.4.

Pia ada hiyo ya paundi milioni 46.5 inamfanya Lacazette aingie kwenye orodha ya wachezaji 10 waliosajiliwa kwa pesa nyingi zaidi na klabu za EPL. Anakamata nafasi ya 7 kwenye orodha hiyo. Nafasi ya kwanza ni ya Mfaransa mwenzie Paul Pogba aliyejiunga na Manchester United mwaka jana kwa paundi milioni 89 akitokea Juventus. Anafuatiwa na Angel Di Maria aliyewahi kujiunga na Manchester United mwaka 2014 kwa ada ya uhamisho paundi milioni 59.5 akitokea Real Madrid.

Nafasi ya tatu ni ya Kevin De Bruyne wa Manchester City aliyejiunga na klabu hiyo mwaka 2015 akitokea Wolfsburg kwa dau la paundi milioni 54.5. Fernando Torres anashikilia nafasi ya nne. Alijiunga na Chelsea Januari 2011 akitokea Liverpool kwa paundi milioni 50. Raheem Sterling ni wa tano kwenye orodha hii ambaye alijiunga na Manchester City kwa paundi milioni 49 mwaka 2015 kutoka Liverpool. Wa sita ni John Stones kutoka Everton ambaye alijiunga na Manchester City kwa paundi milioni 47.5 mwaka jana.

Ni hao sita pekee walionunuliwa na klabu za EPL kwa pesa nyingi zaidi ya Lacazette aliyewahi kuichezea timu ya Taifa ya Ufaransa michezo 11 mbaka sasa. Anafahamika kwa kuwa na kasi, uwezo mzuri wa kiufundi na la muhimu zaidi uwezo wa kupachika mabao utakaowaongezea Arsenal kitu kikubwa mno kwenye msimu ujao wa EPL na mashindano mengine. Aliifungia Lyon mabao 28 msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Ufaransa ambayo ni mengi kuliko mchezaji mwengine yeyote ukimtoa Edinson Cavani wa PSG aliyepachika 35.

Arsene Wenger ameripotiwa kusema kuwa na furaha mno kwa Lacazette kujiunga na klabu yao. Amesema kuwa nyota huyo ameonesha kwa miaka kadhaa kuwa ana uwezo wa kufunga mabao na ni mshambuliaji wa ufanisi wa kiwango cha juu. Kocha huyo wa Washika Bunduki wa London anaamini pia kuwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 ataongeza kitu kikubwa kwenye timu na kuisaidia kuwapa wapinzani ushindani wa kutosha kwenye msimu ujao.

Rekodi za mabao za Alexandre Lacazette ni kipimo kizuri juu ya usahihi wa maneno na imani ya Arsene Wenger. Mabao yake 28 kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa msimu uliopita yaliwaacha mbali washambuliaji nyota kama Radamel Falcao wa Monaco, Kylian Mbappe wa Monaco, Mario Balotelli wa Nice na wengine walioshindwa angalau kuikaribia idadi hiyo. Msimu wa 2014/15 Lacazette alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Ufaransa akifunga jumla ya mabao 27 akiwafunika Zlatan Ibrahimovic, Edinson Cavani na wakali wengine.

Wikiendi hii Lacazette anatarajiwa kusafiri na kikosi cha Arsenal kuelekea Sydney kwa ajili ya michezo ya kirafiki itakayopigwa huko wiki ijayo. Michezo hiyo itafuatiwa na mwingine dhidi ya Bayern Munich jijini Shangai wiki itakayofuata. Mchezo wake wa kwanza katika uwanja wa nyumbani unaweza kuwa kwenye mashindano ya Kombe la Emirates utakaopigwa Julai 29 au 30. Kipimo chake cha kwanza kwenye mashindano rasmi na halisi kitakuwa dhidi ya Chelsea mwezi Agosti kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii.

Ujio wake unatazamiwa kumuondosha kikosini Mfaransa mwenzie Olivier Giroud anayetakiwa na timu kadhaa za EPL zikiwemo Everton na West Ham. Ahadi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Arsenal Ivan Gazidis ya kuleta nyota wa maana kwenye klabu hiyo sasa inaonekana kutekelezwa.

Ifahamike kuwa kwa mujibu wa makubaliano kati ya klabu hizo mbili ada ya uhamisho ya mchezaji huyo ya paundi milioni 46.5 inaweza kupanda mpaka kufikia paundi milioni 53 kulingana na mafanikio atakayopata mshambuliaji huyo ndani ya Arsenal.

Written by Kassim

Exit mobile version