*Chelsea, Man U bado mdororo
*Jua tetesi za usajili wa Ulaya
Mzunguko wan ne wa Ligi Kuu ya England (EPL) umemalizika, ukiwaacha magwiji wawili – Liverpool na Manchester City juu kileleni, huku Watford wakishangaza kwa kuambulia alama moja tu hadi sasa.
Arsenal walitishiwa kupigwa kwa mara ya pili jana Jumapili, lakini walichomoa mabao mawili waliyokuwa wamepigwa na Tottenham Hotspurs kwenye dabi ya London Kaskazini, lakini washambuliaji wake, Alexander Lacazette na Pierre-Emmerick Aubameyang wakasawazisha mambo.
Washika Bunduki wa London walionesha moyo wa ushindani hasa, wakifunga bao muda mfupi kabla ya mapumzikona dakika ya 71. Spurs walitangulia, wakimiliki mpira awali, Christian Eriksen akitia mpira kimiani dakika ya 10 tu kabla ya Harry Kane kufunga kwa penati baada ya kuchezewa faulo na Nahodha wa Arsenal, Granit Xhaka. Kwenye mechi nyingine Jumapili hii, Everton walishinda 3-2 dhidi ya Wolverhampton
Baada ya kukamilika kwa mechi nne hizo, ambazo kwa vyovyote si nyingi nab ado nyingi zitachezwa, timu zimeanza kujigawa ambapo wawili waliomaliza katika nafasi mbili za juu ndio wanaozishikilia, Liver wakiwa na alama 12 kwa kushinda mechi zote na Man City wakiwa nazo 10.
Nafasi sita za juu zinashikiliwa na wawili hao pamoja na Leicester, Crystal Palace, Arsenal na Everton. Chelsea walio kwenye kipindi kigumu cha mpito chini ya kocha Frank Lampard huku wakiwa na marufuku ya kusajili wachezaji. Ni kiangazi cha mwaka huu wamemuuza Eden Hazard kwa Real Madrid.
Chelsea wametupwa katika nafasi ya 11 kwenye msimamo wal ligi huku wababe wengine wa zamani, Manchester United wakishika nafasi ya nane wakiendelea kusuasua chini ya kocha mchezaji wao wa zamani, Ole Gunnar Solskjaer lakini hawapo katika hali njema.
Spurs ambao kwa kawaida huwa kwenye nne bora, wanashika nafasi ya tisa, ambapo uimara wao unaonekana kuporomoka kwa kiasi tangu mwishoni mwa msimu uliopita huku kukiwapo tetesi za kocha wao, Mauricio Pochettino kuondoka, licha ya kwamba alikanusha Jumamosi hii.
Mkiani kabisa wametulizana Watford, wakisaidiwa na Norwich, Aston Villa na Wolves wenye alama tatu kila moja. Brighton, Bournemouth, Newcastle, Southampton na Burnley wana alama nne kila mmoja. Chelsea Sheffield United, Spurs na Man United kila mmoja ana alama tano.
Arsenal anafungana kwa alama saba na Everton, Palace na West Ham wakati Leicester wakiwa wamejikusanyia alama nane. Katika saa za mwisho za usajili Ulaya, AS Roma wanataka kumchukua Henrikh Mkhitaryan wa Arsenal kwa mkopo wa msimu mmoja. Arsenal pia wanatafuta timu ya kumchukua Skhrodan Mustafi.
Barcelona wanasema kukatisha nia yao ya kumrejesha mshambuliaji wao wa zamani, Neymar, kutoka Paris Saint-Germain (PSG). Mazungumzo yalivunjika baada ya PSG kukataa kushusha bei licha ya Neymar kuwa amekubali kulipia pauni milioni 17.7 ili kukamilisha dili hilo.
Real Madrid waliandaa pauni milioni 64 kwa ajili ya kumnasa kiungo wa kimataifa wa Ureno na Sporting Lisbon, Bruno Fernandes, 24. Wanataka pia kumsajili kipa Mfaransa, Alphonso Areola kutoka PSG wakibadilishana na Keylor Navas.
Kiungo Mjerumani wa Bayern Munich, Jerome Boateng anaelezwa kwamba anajiunga na Juventus.