Arsenal wametoka sare ya 2-2 nyumbani kwa Everton katika mchezo mkali ambao hadi dakika saba kabla ya mechi kumalizika, wenyeji walikuwa mbele kwa 2-0.
Timu zote zilishinda mechi zao za kwanza katika ligi kuu hii ya England na Arsenal walitishwa kwenye uwanja wa Goodison Park kutokana na mabao ya kipindi cha kwanza yaliyofungwa na Seamus Coleman na Steven Naismith.
Coleman alifunga baada ya kukokota mpira bila kukabiliwa na wachezaji wa Arsenal alipopokea mpira kutoka kwaGareth Barry. Lile la pili lilifungwa kutokana na mpira wa moja kwa moja wa Romelu Lukaku, ambapo Arsenal watajilaumu kwa kutojifunza kutokana na bao la kwanza.
Hata hivyo, Arsenal waliendelea kupambana na kiungo wake, Aaron Ramsey aliwapa washabiki faraja kwa kufunga bao dakika ya 83 kabla ya mshambuliaji wa kati, Olivier Giroud aliyeingia badala ya Alexis Sanchez kwenye nafasi hiyo kutikisa nyavu dakika ya 90.
Mechi yao iliyopita kwenye uwanja huo Everton waliwanyuka Arsenal 3-0 Aprili mwaka huu lakini katika mechi hii Arsenal walitawala zaidi mchezo na kadiri dakika zilivyokwenda Everton walionekana wazi kuishiwa nguvu.
Arsenal walionesha dhamira ya ushindi kuelekea mwisho mwa mchezo, hali iliyosifiwa na Arsene Wenger huku mpinzani wake, Roberto Martinez akikiri kwamba walikuwa wanaishiwa pumzi, lakini akiwahimiza wachezaji wake kujitahidi wasiruhusu bao, lakini mambo yakashindikana.
Toffees walikuwa na pasi nzuri na kasi wakati wa kushambulia kiasi cha kuwavuka kiungo na walinzi wa Arsenal na kusababisha matatizo golini mwa Gunners lakini hali ilibadilika baada ya Giroud kuingia baada ya nusu ya kwanza na Arsenal wakaanza kuwatesa Everton.
Ramseyalifunga bao kutokana na majalo ya Santi Cazorla wakati Giroud la kwake la kichwa lilitokana na majalo ya Nacho Monreal katika dakika ya mwisho ya mchezo, na kuwasikitisha Everton waliokuwa wameshaamini kwamba wanachukua pointi zote tatu.