*Man City hali ngumu, Liver waua
Mzunguko wa 26 wa Ligi Kuu ya England (EPL) umekamilika kwa matokeo
mchanganyiko, vinara wa ligi hiyo, Leicester wakipnguzwa nguvu.
Wakicheza ugenini kwa Arsenal, Leicester walikubali kichapo cha 2-1,
lakini ndio walioanza kufumania nyavu.
Danny Welbeck aliyerejea kutoka kwenye majeraha ya muda mrefu ndiye
alikuwa shujaa wa mechi kwa kufunga bao la ushindi sekunde za mwisho
za mechi hiyo.
Leicester walibaki wachezaji 10 baada ya kadi ya pili ya njano kwa
Danny Simpson mapema kipindi cha pili, lakini walicheza vyema kwa
kujipanga, chini ya kocha wao, Muitaliano Claudio Ranieri ‘The
Tinkerman’.
Welbeck alikuwa akicheza mechi yake ya kwanza ya kiushindani tangu
Aprili mwaka jana, ambapo aliupokea vyema mkwaju wa adhabu ndogo wa
Mesut Ozil, akafunga baada ya kumzidi maarifa kipa Kasper Schmeichel
na kuamsha ushangiliaji mkubwa Emirates.
Hii ni mechi ya tatu tu kwa Leicester kupoteza. Jamie Vardy ndiye
alifunga bao la kwanza kwa penati baada ya kuonekana kuanguka kutokana
na Nacho Monreal kumnyooshea mguu wake.
Theo Walcott aliingia kipindi cha pili na kufunga bao zuri kutokana na
mpira wa mshambuliaji mwenzake, Olivier Giroud.
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger alisema kwamba alifurahishwa na
ushindi kwa sababu walishinda jaribio gumu kisaikolojia na sasa wapo
kwenye ushindani wa kutafuta ubingwa wa England, kwani wapo pointi
mbili tu nyuma ya vinara Leicester.
MAN CITY WADUWAZWA NA SPURS
Manchester City wanaomsubiri kocha mpya kiangazi kijacho, Pep
Guardiola wamefanya vibaya kwenye mechi yao, wakipoteza kwa Tottenham
Hotspur.
Spurs sasa wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi,
wakifungana pointi na Arsenal, lakini wakiwa na uwiano mzuri zaidi wa
mabao.
Christian Eriksen ndiye alifunga bao dakika za lala salama baada ya
lile la Harry Kane baada ya lile la Kelechi Iheanacho wa Manchester
City.
Huu ni ushindi wa tano mfululizo kwa Spurs, wakionesha kuwa timamu,
kujiamini na moyo wa kupata ushindi chini ya kocha Mauricio
Pochettino.
Manuel Pellegrini alionekana kusikitishwa na vijana wake, kwani tamaa
yake sasa ni kuondoka akiwa amewapa ubingwa kwa mara ya pili. Wamevuna
pointi 26 katika mechi 17 zilizopita, rekodi ambayo bado si nzuri
kulinganisha na ushindani mkubwa uliopo. Wameachwa pointi sita nyuma
ya vinara Leicester wenye pointi 53.
LIVERPOOL WAFANYA MAUAJI
Liverpool wamefanya mauaji kwa Aston Villa kwa kuwakandika mabao 6-0.
Majeruhi wa muda mrefu aliyerejea dimbani, Daniel Sturridge alifungua
kitabu cha mabao, akicheza mara ya kwanza tangu Oktoba mwaka jana.
Mabao mengine yalifungwa na Emre Can, Divock Origi, Nathaniel Clyne,
Kolo Toure. Hii ni mara ya kwanza tangu 1983 kwa Villa kukubali
kichapo cha mabao sita.
Kwa matokeo ya jumla wikiendi hii, Leicester wanashika nafasi ya
kwanza wakifuatiwa na Spurs, Arsenal na Man City.
Mkiani wapo Aston Villa wenye pointi 16, juu yao wapo Sunderland na
pointi 23, moja zaidi ya Newcastle na Norwich.