*Manchester City mikononi mwa Barcelona
Droo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) imetoka, ambapo klabu mbili za England zitakutana na miamba wa Ulaya.
Arsenal waliopoteza mwelekeo katika mechi ya mwisho watakutana na mabingwa watetezi, Bayern Munich.
Vijana hao wa Arsene Wenger walipoteza mechi ya mwisho dhidi ya Napoli ambayo sare tu ingetosha kuwaweka vinara kwenye kundi lao, na sasa watakabiliana na kikosi cha Pep Guardiola.
Manchester City wanaonolewa na raia wa Chile, Manuel Pellegrini watakabiliana na Barcelona ya kocha Gerardo Martino.
Pengine Pellegrini atajilaumu kwa kutomchezesha Sergio Aguero kwenye mechi hiyo, ambapo inadaiwa alidhani kwamba wangeshika nafasi ya kwanza iwapo wangefunga mabao matano dhidi ya Bayern Munich.
Kwa msingi huo alimwacha benchi hata baada ya matatu waliyofunga, akisubiri kama wangefunga la nne amwingize ili apachike la tano. Hata hivyo anadaiwa kumwacha benchi ili acheze dhidi ya Arsenal wikiendi iliyopita.
Wakati hali ikiwa hivyo, Chelsea wamepangwa kukabiliana na Galatasaray wanaofundishwa na Roberto Mancini na ambao wana mchezaji wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba ambaye kocha wa The Blues, Jose Mourinho anamhusudu.
Manchester United wanaelekewa kuwa na ahueni kutokana na kupangwa kukipiga na timu dhaifu ya Olympiakos ya Ugiriki iliyovuka kwa bahati.
Droo hii inadhihirisha jinsi ilivyo muhimu kwa timu kumaliza katika nafasi ya kwanza, ambapo Man U na Chelsea walikamilisha kazi yao mapema.
United
AC Milan wa Italia watakabiliana na Atletico Madrid kutoka Hispania wakati Bayer Leverkusen kutoka Ujerumani watakipiga na Paris St-Germain wa Ufaransa.
Schalke wamepangwa na vigogo wa Hispania, Real Madrid huku Zenit St Petersburg wakipewa wagumu wa Ujerumani, Borussia Dortmund.