*Man U kilio, Man City kicheko
*Villa, Sunderland, Norwich hoi
Arsenal ndio vinara wa Ligi Kuu ya England (EPL) baada ya kuwa na wiki nzuri kitaifa na kimataifa.
Washika Bunduki wa London wameitwaa nafasi hiyo baada ya kuwapiga Aston Villa 2-0 ugenini na kuwaacha vijana wa Remi Garde chini kabisa kwenye msimamo wa ligi.
Arsenal waliofuzu kwa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) katikati ya wiki nchini Ugiriki kwa kuwafunga Olympiakos sasa wanatakiwa kuwa endelevu.
Walipata bao la kuongoza kupitia kwa mshambuliaji wao wa kati Mfaransa, Olivier Giroud ambaye sasa amefikisha mabao 50 kwa klabu hiyo ya London Kaskazini.
Anakuwa mchezaji was aba wa timu hiyo kufikisha idadi hiyo ya mabao, na amefanya hivyo katika mechi 113.
Wengine wa Arsenal waliofunga mabao 50 ni Thierry Henry, Ian Wright, Robin van Persie, Dennis Bergkamp, Robert Pires na Theo Walcott.
Kwa upande mwingine, kipa wa Arsenal, Petr Cech ameweka rekodi ya kutofungwa katika mechi 169 kati ya 349 alizocheza (si kwa Arsenal pekee) akifikia sawa na David James aliyecheza mechi 223 pungufu.
Bao lao la pili walilipata kupitia kwa kiungo mahiri wa Wales, Aaron Ramsey aliyeanzisha na kumaliza kiuzuri shambulizi la kushitukiza. Ramsey ndiye aliyekuwa injini ya ushindi wa Arsenal.
Villa sasa wanahitaji pointi nane ili kuondoka eneo hatarishi la kushuka daraja, wakiwa wameambulia pointi sita tu.
Vijana wa Arsene Wenger, kwa upande mwingine, wameshinda mechi 10 msimu huu na wanaongoza kwa tofauti ya pointi moja, wakiwa nazo 33 wakati Manchester City na Leicester wanazo 32 kila moja na Manchester United wakiwa nazo 29.
City walibahatika kupata ushindi dhidi ya Swansea dakika za mwisho kwani walikuwa sare na kuwasaidia kufikisha pointi hizo.
Katika mechi nyingine za Jumapili hii, Liverpool waliambulia sare ya 2-2 walipowakaribisha West Bromwich Albio wakati Newcastle waliosafiri hadi London Kaskazini walifanikiwa kujinusuru kwenye eneo la kushuka daraja kwa kuwafunga Tottenham Hotspur 2-1 katika hali ya kushangaza.
MANCHESTER UNITED WAPIGWA
Manchester United wamepoteza msingi wao kwenye nafasi za juu za ligi baada ya kutandikwa 2-1 na timu ndogo waliopanda daraja msimu huu, Bournemouth.
Imekuwa wiki mbaya kwa United, kwani wametoka kutolewa katika UCL na Jumamosi wakaishia kupigwa bila matarajio.
Kipa David de Gea atasikitika zaidi kwa makosa, kwani alipigwa moja kwa moja kutokana na kona ya Junior Stanislas, United wakasawazisha kupitia kwa ngongoti wao, Marouane Fellaini lakini wageni wakafunga kupitia kwa mshambuliaji wa zamani wa United, Joshua King kufunga kutokana na mpira wa adhabu ndogo wa Matt Ritchie.
Nusura Bournemouth wapate mabao mawili zaidi kama si Glenn Murray aliyetoka benchi kuzipoteza. Timu hiyo sasa wamepanda hadi nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi baada ya ushindi wa pili mfululizo. Wametoka kuwafunga Chelsea pia.
Kocha wa Manchester United, Louis van Gaal analalamika kwamba angekuwa na washambuliaji wa aina ya Luis Suarez wa Barcelona na Sergio Aguero wa Manchester City wangefunga mabao mengi zaidi msimu huu. Hadi sasa wamefunga mabao sita tu katika mechi saba.
Mshambuliaji wao mpya, Anthony Martial (19) alikosa nafasi mbili za wazi za kufunga lakini pia United walikuwa hovyo kwenye maeneo mengi.
Martial amefunga mabao mawili tu katika mechi tisa wakati alianza kwa makali tangu kusajiliwa kiangazi kilichopita.
Daley Blind ambaye ni ingizo jipya la Van Gaal naye alionekana kucheza hovyo, akiruhusu kuvukwa na bao kuingia kimiani huku akisaidia kidogo sana kwenye kujenga mashambulizi.
MAN CITY NA USHINDI MUHIMU
Kelechi Iheanacho amewasaidia Manchester City kupata ushindi dakika za mwisho, baada ya kuwafunga Swansea wasio na kocha.
City waliofungwa na Stoke kwenye mechi iliyotangulia hivyo kushindwa kujitanua kileleni, walikuwa na wakati mgumu dhidi ya Swansea waliomfukuza kocha wao, Garry Monk Jumatano.
Wilfried Bony wa Man City alimpotezea Ashley Williams na kufunga, lakini Bafetimbi Gomis aliposawazisha ilionekana kwamba mechi ingemalizika kwa sare.
Hata hivyo, katika dakika za mwisho, mchezaji bora wa Afrika kwa kura iliyoendeshwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Yaya Toure alimtengenezea Iheanacho nafasi naye akafunga.
Bao hilo lilikuwa mwiba mchungu kwa Swansea waliokuwa chini ya bosi wa muda, Alan Curtis. Swansea walikuwa na ukame wa mabao kwani hawakupata kufunga katika mechi zao 11 zilizopita.
Katika matokeo mengine wikiendi hii, Norwich walikwenda sare ya 1-1 na Everton, Crystal Palace wakawafunga Southampton 1-0, Sunderland wakalala 0-1 kwa Watford na West Ham wakaenda suluu na Stoke.
Hivi sasa timu tatu zilizo kwenye eneo la kushuka daraja ni Aston Villa wenye pointi sita, Sunderland wenye 12 na Norwich ambao wana pointi 14 sawa na Swansea huku Chelsea wakiwa nazo 15 na kuwa katika eneo hatarishi.