*Hawana kikosi cha ushindi, ni vigumu kukipata
*Wanahitaji nyota watano kurejesha heshima
Siku mpya imeanza na kumalizika katika msimu wa usajili wa majira ya joto, huku Arsenal wakiendelea kuhusishwa na mshambuliaji mwingine tena.
Safari hii ni Luis Suarez, siku chache tu baada ya dunia kujulishwa kwamba Arsene Wenger alikuwa ameamua kuwa kama Harry Redknapp wa QPR alichofanya kwenye dirisha dogo Januari kwa kusajili nyota wengi kwa gharama kubwa.
Wanahabari wakasema kwamba Wenger aliwaambia Liverpool anazo pauni milioni 30 za kumnyakua Suarez, mchezaji hatari na mtata kutoka Uruguay, lakini Liverpool wamekataa ofa hiyo.
Wenger anajulikana miaka mingi kwa sera yake kwenye usajili, na Arsenal wamekuwa wabahili eneo hilo, lakini tunaambiwa tena kwamba wamekataliwa ofa nyingine waliyotoa kwa Bayer Leverkusen kumnasa nyota wao Lars Bender.
Inavyoelekea, mambo mengine yote ni tetesi tu. Si ajabu hakuna hata ofa iliyopelekwa kwa ajili ya Gonzalo Higuain wa Real Madrid; Marouane Fellaini, Wayne Rooney wala Jovetic na wengine wote wanaotajwa kwamba Arsenal wanawataka.
Pamekuwa na maneno mengi sana – kama vile kwamba Cesc Fabregas anarudi kutoka Barcelona, na pia akina Mathieu Flamini, tena bila kulipa ada, lakini yote hiyo imebaki kuwa nadharia tu.
Kinachoonekana kwa vitendo ni kwamba wawili hao wamekataliwa kutolewa mpaka sasa, na kama ilivyotarajiwa, kasajiliwa kijana wa miaka 20, Mfaransa, Yaya Sanogo.
Macho yamewavimba washabiki wa kutupwa wa Arsenal, wamekishangaa ngoja ngoja yao itaisha lini kupata habari za usajili mpya waliotarajia tangu kitambo.
Wanataka kuona mageuzi ya kweli klabuni hapo, kwa ajili ya kuachana na hali ya kuwa washindi wa pili, wa tatu au wa nne, na kurudi tena kuwa mabingwa kwenye mashindano mengi.
Lakini hebu tujiulize, itatokea kweli? Je, Arsenal wanaweza kujidai kwamba ni washindani wa kweli wa kombe lolote miongoni mwa klabu nyingine kubwa zinazojiandaa ipasavyo kiusajili? Wanaweza kuwahakikishia wadau kwamba watakuwa na kikosi cha ushindi?
Kwa miaka minane wamekuwa wakame nyumbani na ugenini, na kwa sababu ya hilo, wachezaji wenye tamaa ya kutwaa vikombe wamegundua hawawezi kuvipata wakiwa na Washika Bunduki wa London, walau kwa aina ya kikosi kilichopo sasa.
Wachezaji nyota wamekimbia Emirates walikolelewa tangu wakiwa wadogo, ambapo kwa hesabu za haraka haraka, wachezaji 23 wa zamani wa Arsenal walioondoka wamefanikiwa kutwaa mataji 56 makubwa katika klabu nyingine.
Kwa upande wa heshima kwa wachezaji hawa, lazima tukiri kwamba kuondoka kwao yametokea kuwa machaguo bora kwa kazi yao na hatima ya maisha yao.
Hata hivyo, inasemwa kwamba sasa mambo yapo tofauti, wanazo fedha! Wana uwezo wa kulipa wafanyakazi mishahara mikubwa na pia kulipa ada ya kufuru ya uhamisho…wana nguvu ya fedha.
Hebu fikiria taswira ya Arsene Wenger akiwa na lile panga la kichawi, akilalamika kwamba bado anasumbuliwa na tatizo lile lile la miaka iliyopita.
Achana na hoja za kiuchumi kwanza, maana hizo zinaeleweka, waangalie wachezaji wenyewe, je, wanaamini kwa dhati kabisa kwamba kwa kujiunga na aina ya kikosi cha sasa cha Arsenal watatwaa mataji?
Tatizo liko hapa; ukweli ni kwamba Arsenal wanahitaji wachezaji wanne au watano wapya wa hadhi ya juu ili kuwa na uwezo wa kushindana kikweli katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ikiwa hali ni hiyo, kwa nini mchezaji yeyote nyota aamue kujiunga nao? Na kwa hali hiyo kunakuwa na mduara ule ule ambao hatimaye unawaacha Arsenal wakiwa weupe.
Bila Arsenal kutangaza usajili wa maana wa walau wachezaji wawili kwa mpigo ili kuonyesha kweli nia yao, hakuna sababu zinazoweza kuwavuta wachezaji wengine nyota kuingia Emirates.
Hiyo ni taswira ambayo kama Arsenal wanataka mafanikio, hawatakiwi kuruhusu kuwa nayo, hivyo lazima waondokane na sintofahamu waliyomo hivi sasa – washindane badala ya kushiriki.
Inasikitisha kwamba hizi sio tena siku zile ambazo wachezaji waligombea kujiunga Arsenal, wakiwa na uhakika kwamba ndani ya miaka mitatu wangerwaa makombe na The Gunners. Wapiganaji hawapo tena, kama wapo wamechoka.
Kwa hali ilivyo wanahitaji ushawishi wa hali ya juu kuja Emirates, maana kuna klabu nyingine kubwa na zenye mvuto na uhakika wa makombe zaidi, wanajua kwamba muda wao wa kucheza soka si mrefu, ujana ukiisha na mpira unaisha.
Ili kupata Arsenal shindani na watakaotwaa makombe, lazima klabu itoe tamko na kuonyesha kwa vitendo wanataka kuwa watu wa namna gani, na waanze na usajili wa nguvu wa nyota wawili.
Bila kunasa sasa saini za wawili hao, kisha kumalizia hao wengine na kuwa na kikosi imara, patakuwa na matumaini gani tena kwamba mabadiliko yatatokea Arsenal na hawatakuwa wale wale wa misimu minane iliyopita?
Manchester United wanaonekana wapo imara, Chelsea imara zaidi na Manchester City wana mkusanyiko wa nyota ambao wanaweza kuchuana na wapinzani wa aina yoyote na kuwachachafya.
Sidhani kuna mchezaji yeyote mmoja mmoja mwenye jeuri ya kusema ni mzuri sana kiuchezaji hivyo kwamab mwenyewe ana uwezi wa kuwainua Arsenal kwenye chati za juu.
Kwa hiyo basi, kabla mchezaji yeyote hajatia saini mkataba wa kuwachezea, watahitaji kuhakikishiwa kwamba hawapo peke yao. Swali linakuja – unawahakikishiaje wachezaji wenye shaka kwamba nyota wengine wanakuja wakati mazingira hayajabadilika?
Na kwa kuanzia, watawashawishije wachezaji wawili wa kwanza kwa kuwaondolewa shaka na wasiwasi wao? Watakubali kweli kuchezea shilingi chooni wakati macho wanayo na hatari wanaijua?
Ukweli ni kwamba Wenger amewasaidia sana Arsenal kwa kuwajengea uwanja, lakini chagizo lake kubwa katika wiki zijazo ni kuitambulisha upya misingi ya klabu yake kwa watu wa nje. Wanataka wachezaji nyota haraka iwezekanavyo ili kujenga kikosi cha ushindi wala si mchezaji mmoja.