*Wawatungua Manchester City 2-0
*West Ham wawacharaza Hull 3-0
Kibao kimegeuka kwa mwinda kuwa mwindwa, na baada ya miaka minne migumu, Arsenal wamefanikiwa kuwacharaza Manchester City nyumbani kwao kwa mabao 2-0.
Arsene Wenger alitumia mfumo tofauti, akichezesha mabeki wanne, mchezaji mmoja mbele yao kisha wachezaji wanne mbele na mmoja akipewa jukumu la kumalizia, naye ni Olivier Giroud.
Alikuwa ni Mfaransa huyo aliyefunga bao la pili kwa kichwa katika dakika ya 67, baada ya mchezaji anayeng’ara vilivyo kwenye kiungo, Santi Cazorla kuwa amefunga bao la kuongoza katika dakika ya 24 ya mchezo.
Arsenal walicheza kwa umakini mkubwa, hasa kwenye ukabaji, kisha wakafanya mashambulizi ya kushitukiza, na katika dakika 20 za kwanza Man City walitawala kwa karibu asilimia 80, lakini Arsenal wanatosheka na kuhakikisha wanalinda lango lao, nyuma akiwapo golikipa David Ospina.
Ni katika mashambulizi ya kushitukiza, beki Nacho Monreal aliyecheza vyema na akina Per Mertesacker, Launrent Koscielny na chipukizi Hector Bellerin alipanda na kuingia ndani ya eneo la penati na Nahodha wa Man City, Vincent Kompany akamchezea rafu iliyozaa penati.
Baada ya bao hilo Arsenal waliendelea na utaratibu wao wa kujilinda na kushambulia kwa kushitukiza, huku mchezaji aliyeitwa kutoka mkopo klabuni Charlton Desemba hii, Francis Coquelin aling’ara akicheza mbele ya beki nne na kuonesha kwa nini Wenger alimrejesha kikosini.
Arsenal wamekatisha mfululizo wa mechi 12 za Man City walizocheza bila kufungwa na ushindi huu ni wa kwanza Etihad tangu Oktoba 2010. Hata hivyo, kwenye ufunguzi wa msimu katika mechi ya Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Wembley, Arsenal waliwafunga City 3-0 na kuitwaa Ngao.
Ushindi huo ni pigo kubwa kwa City, kwani sasa wanakuwa nyuma ya vinara Chelsea kwa pointi tano, baada ya wiki iliyopita tena kwenda sare na Everton. Chelsea wana pointi 52. Arsenal kwa upande wao wamefikisha pointi 39 wakipanda hadi nafasi ya tano, wakiwa pointi moja pungufu ya Manchester United, tatu nyuma ya Southampton.
Katika mechi nyingine Jumapili hii, West Ham wamewafunga Hull 3-0 na kupanda hadi nafasi ya saba baada ya kufikisha pointi 36. Hii ni mara ya kwanza katika mechi tisa vijana wa Sam Allardyce wanafanikiwa kucheza bila kufungwa bao lolote.
Hull wanaonolewa na kocha Steve Bruce wanakabiliwa na majeruhi wengi, ambapo West Ham walitumia udhaifu huo kwa kufunga mabao kupitia kwa nyota wao, Andy Carroll, Morgan Amalfitano na Stewart Downing.
West Ham walikuwa wamecheza mechi nne pasipo kushinda hata moja tangu Krismasi na sasa wanaweza kurejesha tena matumaini ya kuingia kwenye nne bora, japokuwa ushindani ni mkubwa. Kiungo chao kilikuwa imara chini ya Alex Song.
Wapinzani wa Arsenal wa London Kaskazini, Tottenham Hotspur wapo katika nafasi ya sita wakiwa na pointi 37, moja zaidi ya wanaowafuata, West Ham na mbili zaidi ya Liverpool walio nafasi ya nane.
Swansea waliokung’utwa 5-0 na Chelsea wikiendi hii wapo nafasi ya tisa kwa pointi 30 wakati Stoke wanafunga nusu ya juu ya msimamo wa ligi kwa pointi zao 29. Hao wanafuatiwa na Newcastle, Crystal Palace, Everton ambao Jumatatu hii wanacheza na West Bromwich Albion huku nafasi ya 14 wakiwamo Aston Villa.
Walio katika hali tete japo nje ya tatu za kushuka daraja ni West Brom wenye pointi 22, Sunderland wenye 20 sawa na Burnley. Walio mkiani ni Hull na Queen Park Rangers wenye pointi 19 kila mmoja na wa mwisho ni Leicester walioambulia pointi 17 tu hadi sasa.