Arsenal, Real Madrid zang’aa Ligi ya Mabingwa
HATIMAYE mikiki mikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya imeanza, ambapo nyasi zimeanza kuwaka moto.
Kati ya mechi zilizokuwa na mvuto, ni Manchester City dhidi ya Real Madrid na Arsenal dhidi ya Montpellier.
Timu hizo za Uingereza zilikuwa ugenini, ambapo Real walipelekeshana na City puta, na kuja kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dakika ya 90.
Arsenal kwa upande wao, walianza ushiriki wao wa mashindano hayo kwa mwaka wa 15 mfululizo, wakipata ushindi japokuwa hawakucheza vizuri kama kwenye ligi.
Bao la dakika ya 90 la Cristiano Ronaldo wa Real Madrid lilimuwehusha kocha wao, Jose Mourinho ‘The Only One’, aliyechupa kutoka kitini hadi kwenye nyasi, akiteleza kwa magoti kama wafungaji wanavyoshangilia.
Akizungumza baada ya mechi, Mourinho aliyekuwa amejawa furaha alisema Real wanaweza kupoteza mechi, yeye anaweza kupoteza mechi, lakini furaha yake inatokana na kikosi chake kurejesha DNA yake.
Bao la Ronaldo lilihitimisha piga nikupige ya mafahali hao wawili katika dimba la Bernabeu, baada ya golikipa Joe Hart wa Manchester City kufanya kazi ya ziada muda mwingi kuokoa magoli ya wazi.
Matajiri hao wa London walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Edin Dzeko aliyetengewa mpira na Yaya Toure kipindi cha kwanza.
Hata hivyo, vijana hao wa Roberto Mancini walishindwa kujihami, ndipo Marcelo wa Real akasawazisha kwa mkwaju uliomparaza mchezaji wa City kabla ya kumpoteza maboya Hart.
Kiki ya adhabu ndogo ya Aleksandar Kolarov iliwarejesha wageni kwenye uongozi wa mechi na kuwaacha wenyeji wakisikitika.
Alikuwa mshambuliaji mjanja na hatari kwa kushitukiza, Karim Benzema, aliyeachwa kugeuka kwenye eneo la hatari na kuachia fataki iliyomwacha Hart akigaagaa chini.
Wakati Man City wakichukulia mechi ingeisha kwa sare, Ronaldo alimiliki mpira bila kupata wa kumzuia mara moja, na kuukwamisha wavuni, golikipa akiwa kana kwamba amekwenda sokoni.
Kwa ujumla vijana wa Mourinho waliutawala mchezo, na muda mwingi City walikuwa na kazi ya kuutafuta mopira.
Golikipa Hart akizungumza katika mahojiano baada ya mchezo, alionekana kujawa hasira, akisema mipira ilikuwa ikiachwa kuambaa langoni pake kana kwamba watu wa kuiondoa hawakuwapo.
Manchester City wangeshinda wangekuwa wamevunja rekodi ya Real Madrid ya kutofungwa katika mechi za mwanzo za mashindano hayo. Wamechukua kombe mara tisa.
Nchini Ufaransa, Arsenal waliwafunga wapinzani wao kwa mabao 2-1, wakitangulia kufungwa kwa penati ya dakika ya tisa, baada ya nahodha Thomas Vermaelen kucheza rafu eneo la hatari.
Arsenal wanashikilia rekodi ya kupigiwa penati nyingi tangu mwaka 2004, kwani zimefika 11, nyingi kuliko klabu yoyote kwenye mashindano haya.
Hata hivyo, penati hiyo ilikuwa kama kuwachokoza Arsenal, ambao walianzisha mashambulizi ya pamoja, mabeki wakipanda na kushuka kutafuta mabao.
Walikuwa Lukas Podolski na Gervinho waliofanikisha ushindi kwa mabao ya dakika ya 16 na 18, huku golikipa namba mbili, Vito Mannone akiwa imara golini.
Mshambuliaji Mfaransa Olivier Giroud aliyesajiliwa kwa Pauni milioni 13 kutoka Montpellier bado alishindwa kung’ara dhidi ya timu yake ya zamani, kama kwenye ligi, na alitolewa kipindi cha pili.
Wenyeji waliingia dakika 45 za pili wakiwa tofauti kabisa, wakipeana pasi na kufanya mashambulizi ya nguvu.
Arsenal pamoja na ushindi wao walionekana kupwaya kwenye ulinzi, wakifanya makosa ya mara kwa mara, ambapo ni bahati zaidi iliwaepushia kipigo.
Hata hivyo Abou Diaby na Santi Cazorla walifanya kazi nzuri kwenye kiungo, huku kocha Arsene Wenger akitazama kutoka jukwaani, kwani ameanza adhabu ya kutokaa kwenye benchi kwa mechi tatu.
Diaby aliyezawadiwa kadi sekunde ya 21, nusura aisababishie balaa timu yake kwa mchezo mbaya kwenye eneo la hatari lakini refa Carlos Velasco Carballo wa Hispania alipeta.
Yote kwa yote, muhimu kwao ilikuwa kupata pointi tatu walizoondoka nazo kurejea London kujiandaa kukabana na Manchester City Jumapili ijayo kwenye ligi kuu.
Kwingineko katika mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya, AC Milan ilitoka suluhu na Anderlecht wakati Borussia Dortmund wamewafunga Ajax bao 1-0.
Din Zagreb walishindwa kutamba nyumbani baada ya kuadhibiwa na FC Porto kwa mabao 2-0 wakati Malaga waliwakung’uta Zenit Saint Petersburg mabao 3-0.
Olympiakos wakiwa nyumbani nao walikiona cha moto kwa kupokea kipondo cha mabao 2-1 kutoka kwa Schalke 04 wakati Paris SG waliwafunga DyanamoKiev mabao 4-1.
Michezo hiyo inaendelea Jumatano hii kwa Mabingwa wa Ulaya, Chelsea kuwakaribisha Juventus katika uwanja wa Stamford Bridge. Manchester United nao wanajiuliza kwa Galatasaray katika uwanja wa nyumbani wa Old Trafford.
Shakhtar Donetsk wanacheza na FC Nordsiaelland wakati Bayern Munich wanawakaribisha Valencia.
Lille wanacheza na BATE Borisov, Barcelona wakiwakaribisha Spartak Moscow, wakati Braga wakiwavaa CFR Cluj-Napoca.