Hakuna wakati ambao Arsenal walikuwa na nafasi nzuri ya kuwafunga mahasimu wao, Manchester United kama Jumamosi hii, lakini waliendeleza unyonge, tena wakiwa nyumbani kwao.
Kocha wa Man U, Louis van Gaal alipata ushindi wake wa kwanza nje ya Old Trafford jana katika hali ya kushangaza, kwa sababu ana wachezaji wengi wazuri walio majeruhi, na pia beki wake wa pembeni, Luke Shaw aliumia mapema mchezoni na kutoka nje.
Ushindi wa 2-1 walioupata United kutokana na bao la kujifunga mwenyewe la beki Kieran Gibbs na la nahodha Wayne Rooney ulitosha kuwapandisha United hadi nafasi ya nne, huku Arsenal wakiangukia nafasi ya nane.
Mshambuliaji wao aliyekuwa amevunjika mguu, Olivier Giroud alirejea uwanjani kwa mara ya kwanza jana, mwezi mmoja kabla ya muda aliotarajiwa na akafunga bao la kufutia machozi dakika ya 90, akionesha umuhimu wake mbele ya maelfu ya washabiki Emirates waliotarajia ushindi.
Kocha Arsene Wenger alieleza kwamba Arsenal wana tatizo la ulinzi, lakini ni kitu ambacho alikijua tangu wakati wa dirisha la usajili lakini hakujielekeza kwalo, hata baada ya kumuuza beki wa kati na nahodha Thomas Vermaelen.
Gibbs alitia kimiani mwake majalo iliyotoka kwa Antonio Valencia. Arsenal sasa wana pointi 17 tu kutokana na mechi 12, zikiwa ni chache sana katika rekodiya miaka 32, hivyo kuwaweka shakani katika harakati zao za kuusaka ubingwa wa England, kwani wapo pointi 15 nyuma ya vinara Chelsea.
Kipa wa United, David De Gea aliyecheza licha ya kuteguka kidole kidogo cha mkono wa kulia, alikuwa kikwazo kikubwa, ikiwa ni pamoja na kumzuia mchezaji wa zamani wa Man U, Danny Welbeck. Kiungo wa Arsenal, Jack Wilshere naye aliumia na kutolewa nje katika dakika ya 55.
Katika mechi nyingine, Chelsea waliendeleza undava wao kwa kuwafunga West Bromwich Albion 2-0, Everton wakawashinda Aston Villa 2-1, Leicester wakaenda suluhu na Sunderland, Manchester City wakapigana na kuwashinda Swansea 2-1, Newcastle wakapata bao moja bila dhidi ya Queen Park Rangers wakati Stoke waliambulia kichapo cha 2-1 kutoka kwa Burnley.