Menu
in , , ,

Arsenal mwendo mdundo

*Villa, Southampton wakandamiza, Reading doro

Arsenal wameendeleza wimbi la ushindi kupigania nafasi nne za juu, huku Reading wakizidi kuelekea kushuka daraja wakati Aston Villa na Southampton wakijikwamua.
Washika Bunduki wa London sasa wameshinda mechi ya sita kati ya saba zilizopita, huku wakiwashusha Chelsea na kukamata nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL).
Wakicheza ugenini, Arsenal wamewafunga West Bromwich Albion mabao 2-1.
Shujaa wa Arsenal Jumamosi hii alikuwa kiungo wa Jamhuri ya Czech, Tomas Rosicky aliyetupia bao moja moja kila kipindi.
Alifunga bao la kwanza dakika ya 20, kisha akajituma vilivyo na kuokoa bao la wazi lililokaribia kuvuka mstari wa goli baada ya kunasa mpira wa Claudio Yacob.
Rosicky aliyekosa mechi nyingi Arsenal kutokana na kuwa majeruhi siku zilizopita, Jumamosi hii alihaha uwanja mzima kutafuta ushindi, na alipachika bao tena dakika ya 50.
West Brom walipata bao la kufutia machozi katika dakika ya 70 kwa penati iliyogungwa na James Morisson, baada ya beki wa kati, Per Mertesacker kumchezea rafu Shane Long.
Mjerumani huyo alitolewa nje kwa kadi nyekundu, lakini Arsenal waligangamala hadi mwisho na kuchukua pointi tatu muhimu.
Kadi nyekundu ya Mertesacker inahitimisha mfululizo wake kucheza kama beki tegemeo na Arsenal kupata ushindi katika mechi nne mfululizo.
Kutokuwapo kwake kwenye mechi ijayo dhidi ya Norwich kunaweza kutoa nafasi kwa nahodha, Thomas Vermaelen kurejea kuanza kikosi cha kwanza, baada ya kuwekwa kando kutokana na kushuka kiwango.
Kocha Arsene Wenger alimtupa benchi pamoja na kipa namba moja, Wojciech Szczęsny, ambaye Jumamosi hii hata benchi hakuwapo, bali Mtaliano Vito Mannone.
Kwa ushindi huo, Arsenal wamefikisha pointi 56, moja zaidi ya Chelsea na moja pungufu ya Tottenham Hotspurs.
Chelsea wana mechi moja pungufu, Spurs moja zaidi na wote wanacheza Jumapili hii, The Blues wakiwaalika Sunderland na Spurs wakiwakaribisha Everton.
Katika mechi nyingine, Reading chini ya kocha mpya, Nigel Adkins waliadhiriwa na majirani zao wa Southampton kwa mabao 2-0.
Adkins alifukuzwa Saints kabla ya kuajiriwa Reading na hii ilikuwa mechi yake ya pili baada ya ile ya Arsenal. Nafasi yake Saints ilichukuliwa na raia wa Argentina, Mauricio Pochettino anayefanya vyema. Saints walifunga kupitia kwa Jay Rodriguez dakika ya 34 na Adam Lalana dakika ya 72.
Kwa ushindi huo, Southampton wanashika nafasi ya 11 wakiwa na pointi 37 wakati Reading mkiani wamebaki na pointi 23 za muda mrefu, na uwiano wa mabao wa -27, mbaya kuliko wa timu zote za EPL.
Kocha Paul Lambert amefarijika tena kwa timu yake ya Aston Villa kushinda kwa kuwapiga Stoke City 3-1.
Gabriel Agbonlahor alifungua kitabu cha mabao cha Villa lakini Stoke walionesha wapo kwa Michael Kightly kusawazisha dakika 10 kabla ya mechi kumalizika.
Waliodhani ingekuwa sare walikosea, kwani Matthew Lowton aliwanyanyua washabiki wa Villa dakika ya 87 kabla ya kinara wao wa upachikaji mabao, Christian Benteke kuandika bao dakika ya 90.
Villa wamejiondoa kidogo eneo la kushuka daraja, kwani sasa wanashika nafasi ya 16 kwa pointi 33.
Mechi pekee iliyoambulia sare ilikuwa ya Norwich waliowakaribisha Swansea na kutoshana nguvu kwa mabao 2-2.
Wageni walitangulia kupata bao kupitia kwa Miguel Michu dakika ya 35 kabla ya Robert Snodgrass kusawazisha dakika ya tano tu baadaye. Michael Turner wa Norwich alibadili kibao dakika ya 60, lakini Swansea waliwang’ang’ania kwa kusawazisha dakika 15 baadaye, kupitia kwa Luke Moore.
Matokeo hayo si mazuri kwa Norwich waliojenga mazoea ya kufungwa siku za karibuni, kwani yanawatupa nafasi ya 13 wakia na pointi 35 wakati swansea wapo ya tisa kwa pointi 41.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version