*Man City wabanwa
Arsenal wamepata pigo kubwa baada ya kucharazwa mabao 5-1 na Liverpool kwenye dimba la Anfield.
Arsenal waliokuwa wanaongoza ligi waliingia kwenye mechi hiyo wakitarajia kuongeza pointi lakini walionekana wachovu.
Tangu mwanzo hali ya hewa ilionekana kuwaenda kombo vijana hao wa Arsene Wenger, ambapo ndani ya dakika 20 walishafungwa mabao manne.
Mabao ya Liverpool yalifungwa na Martin Sktel dakika ya kwanza na ya 10, Raheem Sterling ya 16 na 52 na Daniel Surridge dakika ya 20. Arsenal walipata la kufutia machozi dakika ya 69 kwa penati ya Mikel Arteta.
Arsenal wanatakiwa wajijenge kisaikolojia kabla ya mechi yao Jumatano dhidi ya Manchester United dimbani Emirates kabla ya kuwakaribisha tena Liverpool katika raundi ya tano ya Kombe la FA.
Katika mechi nyingine, Manchester City waliofungwa na Chelsea 1-0 majuzi, walishindwa kufurukuta walipokuwa wageni wa Norwich, wakatoa 0-0.
City wangeshinda wangekamata nafasi ya kwanza lakini vijana wa Manuel Pellegrini walionekana bado kuwa na bumbuwazi kutokana na kipigo cha Chelsea Jumatatu iliyopita.
Chelsea nao waliendeleza wimbi la ushindi kwa kuwakandamiza Newcastle 3-0 na kuchukua uongozi wa ligi baada ya kufikisha pointi 56.
Arsenal wanakuwa wa pili kwa pointi 55 na City wa tatu kwa pointi 54 wakifuatiwa na Liverpool wenye pointi 50.
West Ham waliwafunga Aston Villa 2-0, Crystal Palace wakawalaza West Bromwich Albion 3-1, Southampton wakaenda sare ya 2-2 na Stoke, Sunderland wakafungwa na Hull 2-0 huku Swansea wakiwakung’uta wapinzani wao wa jadi Cardiff 3-0.
Nafasi tatu za mwisho zinashikwa na West Brom wenye pointi 23, Cardiff 21 na Fulham 19.