Menu
in , , ,

Arsenal matawi ya juu

*Di Canio balaa, awatungua Everton kweupe
*Reading, Wigan, QPR waelekea kuaga EPL

Mzunguko wa 33 wa Ligi Kuu ya EPL umeshuhudia Arsenal wakichupa tena nafasi ya tatu, baada ya kuwafunga Fulham 1-0.
Pamoja na ushindi, Arsenal hawakuonesha cheche kali, licha ya wenyeji Fulham kucheza 10 kwa zaidi ya dakika 80, baada ya Steve Sidwell kupewa kadi nyekundu kwa mchezo mbaya dhidi ya Mikel Arteta.
Beki wa kati wa The Gunners, Mjerumani Per Mertersacker alifunga bao pekee kwa kichwa dakika ya 43 na kuwahakikishia vijana wa Arsene Wenger ushindi muhimu, kwenye vita ya kupata nafasi Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Olivier Giroud atajilaumu mwenyewe kwa rafu mbaya dhidi ya dakika za mwisho mwisho, hivyo kuzawadiwa kadi nyekundu. Fulham wanashika nafasi ya 11 kwa pointi 40 wakati Arsenal wanazo 63.

DI CANIO ANGURUMA TENA

20130331-191707.jpg

Himaya ya Paolo Di Canio inaelekea kupata nguvu ya pekee, na sasa washabiki wameanza kuliimba jina lake kutokana na mafanikio.
Mtaliano huyo amefurahia ushindi wa pili tangu ashike usukani, ukiwa ni wa kwanza nyumbani, walipowasasambua Everton kwa bao 1-0.
Ushindi huo unawaweka Sunderland nafasi ya 14, wakiwa na pointi sita nje ya eneo la hatari, lakini unawaumiza Everton wa David Moyes, waliokuwa wakifurukuta nao washiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Bao la Sunderland lilifungwa na mchezaji wao mahiri, Stephane Sessegnon katika nusu ya kwanza ya mchezo, baada ya pasi mkaa ya Leighton Baines kunaswa na Sebastian Larsson aliyempelekea mfungaji. Everton wana pointi 56 katika nafasi ya sita.

READING, WIGAN, QPR MAJI YA SHINGO

Panga la kushuka daraja limeendelea kuzielekea timu tatu zilizokuwa mkiani, Reading, Wigan na Queen Park Rangers (QPR), baada ya kuvurunda na kupoteza mechi za Jumamosi hii.
Norwich City hatimaye walipata ushindi baada ya mechi nyingi za sare na kufungwa, na wanyonge wao walikuwa Reading, waliowafunga 2-1 na kujinasua eneo la hatari kubwa.
Wakati Norwich wamefikisha pointi 38 wakishika nafasi ya 13, Reading wameendelea na sifa ya kuburuza mkia, kwa pointi zile zile 24 na uwiano mbaya wa mabao -28.
Wigan ambao huzinduka mwisho wa msimu wanaelekea kuzidiwa na usingizi hadi hatua hii, ambapo wamepoteza mechi mkononi mwa West Ham United wenye uhakika wa kubaki EPL.
West Ham wanaofunzwa na Sam Allardyce walipata mabao mawili na pointi tatu zilizowafikisha nafasi ya 10 na akiba ya pointi 42 huku Wigan ambao hawakupata bao lolote wakiwa nafasi ya 18 kwa pointi 31.
QPR wa Harry Redknapp kwa upande wao, walikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Stoke City waliokuwa pia wakisumbuliwa na hatari ya kushuka daraja msimu huu.
QPR sasa wanashika nafasi ya pili kutoka mwisho wakiwa na pointi 24 sawa na Reading, wakiwa na afadhali ya bao moja tu kiuwiano wakati Stoke wanaofundishwa na Tony Pulis wapo nafasi ya 15.
QPR watatangazwa rasmi kushuka daraja iwapo Aston Villa watawafunga Manchester United katika mechi ya Jumatatu jioni, vinginevyo wataendelea kusubiri mechi zijazo.

NEWCASTLE WAENDELEA KUSUASUA

Msimu umeendelea kutochanua kwa Newcastle United, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na West Bromwich Albion.
Wadau wa Newcastle wameendelea kuwa na wasiwasi iwapo hawatashushwa daraja, kwani mwenendo wao umekuwa si mzuri na iwapo timu za mkiani zitaibuka na kushinda mechi zijazo, watakuwa hatarini.
Vijana hao wa Alan Pardew wanashika nafasi ya 16 wakiwa na pointi 37 wakati West Brom wapo nafasi ya nane kwa pointi zao 45.

SOUTHAMPTON WAENDELEZA UGUMU

Southampton waliokaa kwa muda mrefu katika nafasi za kushuka daraja kabla ya kujinasua, wameendeleza wimbi la kutofungwa mechi za EPL.
Wamecheza na Swansea City, ambayo imekuwa mechi ya sita mfululizo kutofungwa, na ilikuwa ngumu kupata pointi moja huko Wales walikochezea.
Matokeo hayo yanaziacha timu zote maeneo salama, kwani Southampton wana pointi 39 katika nafasi ya 12 na Swansea wapo nafasi ya tisa kwa pointi 42 walizojikusanyia katika mechi tisa.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version