Menu
in , , ,

Arsenal: Mapinduzi baada ya Arsène Wenger

AW

Miaka miwili imepita tangu kung’atuka kwa kocha wa muda mrefu wa Arsenal, Arsene Wenger, na mapinduzi yanaanza kuonekana.

Miaka yake ya mwisho ilikuwa ya tabu, ya kuboa na kukatisha tamaa miongoni mwa washabiki kindakindaki wa klabu hii ya London Kaskazini, ambayo katika miaka ya awali ya kocha huyu Mfaransa, walipata mafanikio.

‘Ufalme’ wa Wenger ulikuwa wa aina yake, akiwa nguzo na wakati mwingine akigeuka kuwa kama taasisi hasa, lakini uasi ulianzia kwa washabiki, wakashika mabango, wakaandamana, wakarusha ndege – mabango yakiwa ni ‘Wenger Out’, lakini akakomaa na wamiliki wakabaki kumuunga mkono.

Ilikuwa wiki kama hii miaka miwili iliyopita ‘Profesa’ Wenger alipoamua kuachia ngazi na kusema ‘kwa herini’ na sasa anakula bata kwenye Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA). Ilifika mahali washabiki wakachoka hata juu ya sauti zao wenyewe. Klabu ya soka inaweza kuwa chombo cha kubeba hisia na mihemko tofauti – raha na hasira, upendo na chuki, lakini kwa Arsenal kila kitu kilionekana kushika ganzi, vikigota kwenye mzunguko wa matumaini na masikitiko.

Mikel Arteta
Mikel Arteta

Kama alivyopata kuandika Raymond Chandler, kusema kwa heri ni kufa kidogo. Lakini Wenger alipotangaza kuondoka, kidogo kidogo Arsenal walianza kuwa klabu wanaozaliwa upya, kwani kwa miaka mingi klabu ilikuwa kama ya mtu mmoja katika Wenger, uhafidhina ukazidi na wadau kuchoka, ikiwa ni pamoja na wachezaji waliokuwa na kiu ya mataji.

Walianza kuondoka taratibu kwenye ramani ya Ulaya, wakakosa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), wakawa sasa wao ni wa ile ligi ndogo – Ligi ya Europa. Lakini tangu alipoondoka ikawa ni fursa nzuri ya kuanza kubadilisha mamb, kuteka na kuwa na nguvu na utambulisho mpya.

Yamekuwa sasa kweli ni mapinduzi dhidi ya utamaduni uliojengwa na mtu mmoja kwa miaka mingi, licha ya nguvu ya fedha waliyokuwa nao na miundombinu mizuri, klabu walionekana kushuka badala ya kupanda.

Mapinduzi ya kweli sasa yanaonekana baada ya nafasi ya Wenger kuchukuliwa na Unai Emery na kisha mchezaji na nahodha wao wa zamani, Mikel Arteta – misingi ya Wenger inavunjwa hatua kwa hatua kwenye kila ngazi ya klabu, wakibadili mambo, ikiwa ni pamoja na kuwa na maofisa zaidi kama mkurugenzi wa ufundi na soka, vitu ambavyo Wenger alipiga vita, akitaka abaki mwenyewe kushika hatamu.

Wamiliki na viongozi wakaja kubaini kwamba walikuwa katika hali mbaya kwenye miaka ya mwisho ya Wenger ambaye ni dhahiri kwamba alikaa madarakani kwa muda mrefu mno na kuwa na mamlaka makubwa kupita kiasi, licha ya ukweli kwamba amewapa rekodi iliyoshindikana kuvunjwa – kutofungwa mechi hata moja katika msimu wa 2003/2004.

Sasa DNA ya Arsenal inabadilika kabisa; mabadiliko ni mengi na ya haraka, ikiwa ni pamoja na jopo la ufundi na baadhi ya viongozi, Ivan Gazidis aliyekuwa amepewa mamlaka ya kusimamia mabadiliko akakimbilia AC Milan miezi mitano tu baadaye, akiacha alama ya vidonda vilivyo wazi.

Alikuwa amemuahidi Sven Mislintat ‘Jicho la Almasi’ la klabu linalojua kung’amua vipaji, nafasi ya ukurugenzi wa ufundi. Aliingia pia Raul Sanllehi na sasa Edu na Arteta – klabu inaonekana inakwenda kwenye mkondo sahihi na taratibu matokeo yataanza kuwa dhahiri.

Arsenal walionekana kuwa dhaifu na taratibu Arteta anawarudisha kwenye reli – akijaribu kuondoa udhaifu uliokuwa hap ana pale uwanjani, hasa kwenye eneo la ulinzi. Nyota ya Arsenal ilianza kuonekana kung’aa vizuri muda mfupi tu kabla ya mechi za Ligi Kuu ya engand (EPL) kuahirishwa kutokana na viruso vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu.

Watu wanaweza kusema kwamba uwapo wa Emery ulikuwa kupoteza muda, lakini ukweli ni kwamba alikuwa muhimu na akawa kama utenganishi wa yale ya kale na mapya. Kikawa kipindi cha mpito na sasa wanakwenda vyema chini ya kocha kijana, anayewajaza wachezaji wake nguvu na kuwapa washabiki matumaini mapya.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version