Arsenal wamefanikiwa kuvuka giza la kupoteza mechi mbili mfululizo, kwa kuibuka na ushindi dhidi ya West Bromwich Albion, huku Manchester United waking’ara dhidi ya Hull.
Wakicheza ugenini, Arsenal walikuwa kama nguvu sawa na wenyeji wao hadi saa nzima ilipotimia, ambapo alikuwa Danny Welbeck aliyezifumania nyavu kwa kupiga kichwa cha nguvu kilichozama golini.
Welbeck alifunga kufuatia majalo ya Santiago Cazorla na bao hilo lilitosha kuwahakikishia Washika Bunduki wa London wanapata pointi zote tatu. Mechi iliyopita walifungwa na Manchester United wakati iliyotangulia walifungwa na Swansea.
Hata hivyo uhai wao ulianza wiki iliyopita walipowachabanga Borussia Dortmund 2-0 kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kurejea kwa beki wa kati mahiri Mfaransa Laurent Koscielny kunaonekana kuwapa nguvu kubwa, akicheza sambamba na Per Metersacker.
Arsenal walianza mechi hiyo wakiwa na pointi chache kuliko ilizopata kuwa nazo katika michezo 12 katika miaka 32 iliyopita, lakini kocha Arsene Wenger anasema kwamba huu ni mwanzo mpya na kwamba wachezaji wanaendelea kujifunza.
Mashabiki wachache wa Arsenal walionesha mabango yanayomtaka Wenger aondoke, lakini yakimshukuru kwa mazuri aliyofanya. Welbeck alicheza pembeni ya Olivier Giroud aliyerejeshwa kwenye namba tisa yake baada ya kuwa nje kwa kuvunjika mguu.
MANCHESTER UNITED WACHEKELEA USHINDI
Manchester United walipata ushindi mzuri wa 3-0 dhidi ya Hull, lakini walipata pigo kwani kiungo wao aliyevunja rekodi ya usajili, Angel Di Maria alitoka nje dakika ya 13 tu kwa kuumia mguu.
Mabao ya United yalifungwa na Chris Smalling, Wayne Rooney na Robin van Persie, aliyefanikiwa kupata bao baada ya ukame wa mwezi mzima. Alitolewa nje baadaye, akaingia Radamel Falcao, ambaye amekuwa nje kwa maumivu kwa wiki sita.
Hull wamefungwa mechi nne mfululizo sasa na kocha Steve Bruce anatakiwa kuwasuka zaidi vijana wake ili kuepuka kutumbukia kwenye eneo la kushuka daraja. Hadi sasa wamefanikiwa kushinda mechi moja tu.
MATOKEO MENGINE YA LIGI KUU
Katika matokeo mengine, Chelsea walibanwa na Sunderland kwa kwenda suluhu, Burnley wakaenda sare ya 1-1 na Aston Villa, Liverpool wakawafunga Stoke 1-0, Queen Park Rangers (QPR) wakashinda 3-2 dhidi ya Leicester, Swansea na Crystal Palace wakaenda 1-1 huku West Ham wakiwapiga Newcastle 1-0.
Kwa matokeo hayo, Chelsea wanaendelea kuongoza wakiwa na pointi 33 wakifuatiwa na Southampton wenye 26, Manchester City wenye 24 na Man United waliofikisha 22. West Ham wanafuata kwa pointi 21 na Arsenal kwa pointi moja pungufu.
Nafasi ya saba inashikwa na Swansea wenye pointi 19 sawa na Newastle, wakati Everton, Tottenham na Liverpool wamefungana kwa pointi 17. Stoke wapo nafasi ya 12 wakifuatiwa na Sunderland, Crystal Palace, West Brom, Aston Villa na Hull.
Walio katika eneo la hatari la kuweza kushuka daraja kwa sasa ni QPR wenye pointi 11 sawa na Hull, nafasi ya 19 inashikwa na Burnley wenye idadi hiyo hiyo ya pointi wakati mkia unaburutwa na Leicester.