Mzunguko wa tisa wa Ligi Kuu ya England umeibua ushindi muhimu kwa baadhi ya timu na nyingine kuzidi kunyong’onyea.
Arsenal katika mechi ya awali kabisa Jumamosi hii walikumbana na kigingi cha timu inayoshika nafasi ya pili kutoka mkiani, Crystal Palace lakini hatimaye waliibuka na ushini.
Vijana hao wa Arsene Wenger walianza mechi kwa kujiamini, lakini Palace walioachana na kocha wao Ian Holloway waligangamala na kudhamiria kupata ushindi katika uwanja wao wa nyumbani.
Hadi mapumziko mambo yalikuwa suluhu, na kipindi cha pili Arsenal walianza kwa kasi, wakimtumia pia kinda Mjerumani, Serge Gnabry aliyeingia mapema kipindi cha kwanza badala ya Mathieu Flamini aliyeumia.
Gnabry alikuwa akiambaa ambaa katika eneo la penati ndipo akafaniwa rafu mbaya na nahodha msaidizi, Mikel Arteta akafunga penati iliyofufua matumaini ya Arsenal.
Hata hivyo, Washika Bunduki wa London waliendelea kuandamwa na Arteta alitolewa nje kwa kadi nyekundu yenye utata kwa madai ya kumkwatua Marouane Chamack aliyekuwa akichanja mbuga kwenda kufunga.
Olivier Giroud alipata bao katika robo ya mwisho ya mchezo baada ya majaribio mengi na kuwahakikishia The Gunners kubaki kwenye usukani wa ligi hiyo.
Katika mechi nyingine, Manchester United walianza kinyonge dhidi ya Stoke, na katika robo ya kwanza walishalala kwa bao moja, walilokomboa baadaye kupitia kwa Robin van Persie lakini wakafungwa tena la pili muda mfupi baada ya hapo.
Wakicheza nyumbani, kocha wa Man U, David Moyes alionekana kuchanganyikiwa na matokeo mabaya, na kadiri muda ulivyokwenda Stoke walielekea kuchoka na Manchester wakasawazisha kupitia kwa Rooney kisha kuongeza bao la tatu kupitia kwa Javier Hernandez ‘Chicharito’ na kuwa faraja kubwa kwa umati wa washabiki Old Trafford.
Liverpool kwa upande wao waliendelea kufanya vizuri, ambapo waliwafunga West Bromwich Albion mabao 4-1, baada ya Luis Suarez kufunga mabao matatu na mshambuliaji mwenzake, Daniel Sturridge kuweka moja.
Katika mechi nyingine, Norwich walikwenda suluhu na Cardiff wakati Southampton waliwapiga Fulham 2-0.
Aston Villa walipoteza mechi nyumbani kw akufungwa 2-0 na Everton.
Arsenal wanaendelea kuongoza ligi kwa tofauti ya pointi mbili wakifuatiwa na Liverpool, Southampton na Everton.
Jumapili hii, wanaoshika nafasi ya tano na sita, Chelsea na Manchester City wanakipiga katika mechi yenye mvuto mkubwa.
Nafasi tatu za mwisho zinashikwa na Norwich wenye point inane, Palace wenye pointi tatu na Sunderland wenye pointi moja.
Sunderland nao watacheza na Newcastle ambao ni mchezo wa watani wa jadi, Swansea watawavaa West Ham na Tottenham Hotspur watacheza na Hull.
Katika mechi ya El Classico nchini Hispania, Barcelona walifanikiwa kuwafunga mahasimu wao wa kitaifa, Real Madrid kwa 2-1 kupitia mabao ya Neymar na Alex Sanchez wakati Madrid walifunga kupitia kwa Jesse.