*matusi ya mashabiki wa Arsenal siwezi kuyarudia hapa*
Arsenal wameanza msimu mpya wa Ligi Kuu ya England (EPL) vibaya nyumbani kwao kwa kuchapwa 2-0 na West Ham.
Walitarajiwa kuwa wazuri kutokana na kuwa na maandalizi mazuri ya kabla ya msimu lakini waliwaangusha washabiki wao katika kile kocha wao, Arsene Wenger alichosema kuwa ni ajali.
Wenger ameahidi kwamba kutokana na matokeo hayo, wataanzia hapo na kujijenga vyema katika harakati za kuwania taji la EPL, lakini alisema wachezaji wake waliruhusu mabao kirahisi.
West Ham walipata ushindi wa kwanza wa ligi chini ya kocha mpya, Slaven Bilic aliyepata kuchezea timu anayofundisha lakini ambaye pia ni mwanafunzi wa Wenger.
Licha ya kufungua vyema pazia la msimu kwa kuwafunga Chelsea wikiendi iliyopita, Arsenal walishindwa kufanya walichotarajiwa. katika mchezo nilioushuhudia mwenyewe ‘LIVE’.
Kipa wa zamani wa Chelsea aliyejiunga Arsenal, Petr Cech alionekana kukosea uamuzi juu ya mpira wa adhabu wa Dimitri Payet kiasi cha kumruhusu Cheikhou Kouyate kutia bao la kwanza dakika mbili kabla ya mapumziko.
Licha ya Arsenal kumiliki mpira kwa asilimia 62, walijikuta wakiadhibiwa tena katika kipindi cha pili, baada ya Mauro Zarate kufumania nyavu kwa shuti lililotoka yadi 20 na hiyo ilitokana na kutokuwa makini kwa walinzi wa Arsenal.
Washabiki wa Arsenal walianza kuondoka kwa wingi kabla ya kipenga cha mwisho, baada ya kuona kwamba mechi yao ya kwanza ya msimu imeanza vibaya, nikiwa mmoja wao.
Arsenal watatarajia kwamba walau kabla ya dirisha la usajili kufungwa wataongeza mshambuliaji mmoja wa kusaidiana na Olivier Giroud, na macho na masikio yapo kwa Karim Benzema wa Real Madrid.