*Chelsea chali, Mourinho matatani tena
*Leo ni Manchester United na Man City
Arsenal wamepata ushindi muhimu kwenye mechi ya ugenini dhidi ya Everton na kuchupa hadi nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL).
Kocha Arsene Wenger amewamwagia sifa wachezaji wake, akiita ni wiki iliyokuwa tamu mno kwake, kwani katikati ya wiki walitangulia kuwafunga Bayern Munich 2-0 kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
Wakicheza huku theluji ikianguka Goodison Park, Arsenal walifanikiwa kupata bao la kwanza kupitia kwa mshambuliaji wa kati Mfaransa, Olivier Giroud dakika ya 36, baada ya Mesut Ozil aliyeonesha kiwango cha juu kuachia majalo nzuri. Ozil ndiye alikuwa mchezaji bora wa mechi hiyo.
Dakika mbili tu baadaye, beki wa kati kisiki, Laurent Koscielny alifunga kwa kichwa baada ya kuupokea vyema mpira wa kiungo Santi Cazorla, akiwaacha wachezaji wa Everton na kipa wao, Tim Howard wakishangaa na kusikitika.
Hata hivyo, dakika moja kabla ya mapumziko Ross Barkley alisawazisha bao na muda mfupi baadaye mshambuliaji machachari wa Everton, Romelu Lukaku alipoteza nafasi nzuri na ya nadra sana, ambapo mpira wake wa kichwa uligonga mtambaa wa panya.
Kipa wa Arsenal, Petr Cech, alionesha umahiri wake na jinsi alivyo hazina kwa klabu iliyomsajili kiangazi kilichopita, pale alipookoa hatari kadhaa, ikiwamo moja ya Gerard Deulofeu.
Jumamosi hii iliendelea kuwa mbaya, kwani katika dakika za majeruhi, Gareth Barry alipewa kadi nyekundu, baada ya kupewa kadi mbili za njano na kutolewa nje kutokana na kumchezea vibaya Kieran Gibbs ambaye aliingia uwanjani dakika ya 89 kuchukua nafasi ya Alexis Sanchez.
Wenger alishindwa kuizuia furaha yake, akisema lazima wawe na uendelevu katika kiwango chao, kufanya kazi pamoja kwa unyenyekevu na kwamba anaionea fahari timu yake kwa sababu wameonesha uwezo wao na kujielekeza inavyotakiwa. Kuendelea kuongoza ligi kutategemea matokeo ya wababe wa Manchester Jumapili hii, kwani Man City wana pointi 21, moja pungufu ya Arsenal na United wanazo 19.
CHELSEA WAPIGWA, MATIC NA MOURINHO NJE
Chelsea wameendelea na hali mbaya kabisa kwenye EPL, baada ya kukubali kichapo cha 2-1 kutoka kwa wenzao wa London, West Ham, huku kiungo Nemanja Matic na kocha Jose Mourinho wakitolewa uwanjani kwa nidhamu mbaya.
Chelsea waliotawala zaidi mechi hiyo, walianza kuadabishwa baada ya Mauro Zarate kufunga bao kutokana na Chelsea kushindwa kufagia mpira wa kona katika dakika ya 17. Mlinzi Gary Cahil alisawazisha bao katika dakika ya 56 akipokea majalo ya Willian baada ya mpira wa kona kupigwa.
West Ham walipata bao la ushindi katika dakika ya 78 kwa Andy Carroll kupiga kichwa kizuri akiwa katikati ya kasha la penati, akiutendea haki mpira wa Aaron Cresswell. Kwa ushindi huo, West Ham wamepanda hadi nafasi ya tatu baada ya kufikisha pointi 20, lakini kubaki hapo kutategemea mechi ya Man United na Man City Jumapili hii, kwani United wana pointi 20.
Chelsea walionesha utovu wa nidhamu, ambapo wachezaji wake walioneshwa jumla ya kadi sita za njano na moja nyekundu kwa Matic; kadi ya pili ya njano akiipata kutokana na kumchezea vibaya Diafra Sakho.
Kadi hiyo nyekundu ilisababisha mzozo, ambapo wachezaji wa Chelsea walikurupuka kuipinga na ni hapo Diego Costa na Cesc Fabregas walipopewa kadi zao za njano. Mourinho naye alielekezwa kwenda kukaa majukwaani badala ya kwenye eneo la ufundi, baada ya kumfuata mwamuzi Jon Moss chumbani kuzungumza naye wakati wa mapumziko.
Wakati bao la ushindi la West Ham linafungwa, Mourinho alinaswa akiwa amesimama katikati ya washabiki wa West Ham, lakini muda mfupi baada ya hapo alitoweka, asionekane tena jukwaani.
Kadhalika, kocha msaidizi wa kikosi cha kwanza cha Chelsea, Silvino Lauro alitolewa nje kwa nidhamu mbovu. Sasa Chelsea wamepoteza mechi tano kati ya 10 walizocheza za EPL msimu huu, wakiwa na pointi 11 tu huku wakishika nafasi ya 15.
Hii ilikuwa mechi ya mwisho kwa West Ham kucheza na Chelsea katika dimba la Upton Park, kwani wanatarajiwa kuhamia Olympic Stadium kiangazi kijacho.
MATOKEO YA MECHI NYINGINE ZA EPL
Katika mechi nyingine za EPL Jumamosi hii, Aston Villa walilala 2-1 kwa Swansea na kuongeza machungu kwa kocha Tim Sherwood ambaye kibarua chake kipo hatarini kutokana na mwenendo mbaya wa timu msimu huu.
Villa walicheza nyumbani wakitarajia kupata walau pointi moja, lakini walishindwa, hivyo kubaki katika nafasi ya 19 kwenye msimamo wa ligi, ambapo kwenye mechi zote 10 wameambulia pointi nne tu.
Leicester walitumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kuwafunga Crystal Palace 1-0 na Leicester wanashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi, wakionekana kufufuka sana tangu walipomwajiri kocha Mwitaliano, Claudio Ranieri kiangazi kilichopita.
Norwich waliendelea na maumivu yao, kwani wakichezanyumbani walilala 1-0 mbele ya West Bromwich Albion. Norwich wapo nafasi ya 16, yaani moja nyuma ya Chelsea wakati West Brom wamepanda hadi ya nane kwenye msimamo wa ligi.
Stoke walifungwa na Watford 2-0 na kushuka hadi nafasi ya 14 wkaati Watford waliopanda daraja msimu huu wakipanda mpaka nafasi ya 13.
Mechi nyingine leo hii ni Sunderland wenye kocha mpya Sam Allerdyce watacheza na Newcastle katika ‘derby’ ya eneo hilo. Itakumbukwa kwamba Sunderland wanashika mkia wakiwa na pointi tatu tu huku Newcastle wakishika nafasi ya 18 na pointi zao sita.
Kadhalika kuna mechi nyingine kubwa, ambapo kocha mpya wa Liverpool, Mjerumani Jurgen Klopp atakuwa na kazi ya kuwawezesha vijana wake kukabiliana na wageni Southampton.