* Man Utd yapoteza kwa Southampton
*Arsenal yainyanyambua Stoke City
Baada ya kuonekana kama mambo yanataka kutengemaa kwa Manchester United huku wakivuna pointi 37 na kushika nafasi ya tatu baada ya mechi 20, leo mambo yamegeuka na kujikuta wakiruhusu kichapo cha bao 1-0 wakiwa Old Trafford dhidi ya Southampton na kushuka hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kuu Uingereza.
Bao pekee kutoka kwa kiungo mshambuliaji wa Southampton, Dusan Tadic lililopatikana kipindi cha pili, lilitosha kuwapatia alama tatu muhimu vijana wa kocha Ronald Koeman ambao msimu huu wanaonekana kuwa moto wa kuotea mbali.
Pointi hizo muhimu za leo zimewapeleka hadi kwenye nafasi ya tatu baada ya kutimiza alama 39 kutokana na mechi 21 walizocheza hadi sasa. Tofauti na wengi walivyodhani, Southampton ndiyo timu iliyoruhusu kufungwa mabao machache mpaka sasa kuliko timu yoyote (mabao 15 pekee) licha ya kuuza watu kama Dejan Lovren.
Pamoja na kuonyesha kupambana, Manchester United hawakuweza kulenga hata shuti moja golini na hii ni dalili tosha kuwa safu ya ushambuliaji ya vijana wa kocha Loius Van Gaal hawakuwa katika ubora kwenye mchezo wa leo licha ya kumiliki mpira kwa asilimia 60.
Kwa upande wa pili, leo kulikuwa na mchezo mwingine pale katika dimba la Emirates ambapo Arsenal walikuwa nyumbani kuwaalika Stoke City na mchezo huo umemalizika kwa Arsenal kupata ushindi wa mabao 3-0.
Alexies Sanchez aliendelea kuwa Mfalme wa magoli kwa upande wa Arsenal baada ya kufunga mabao mawili na kufikisha jumla ya mabao 12 ya ligi kuu msimu huu huku lile la tatu, likifungwa na beki wa kati, Laurent Conscienly.
Wachezaji wa Southampton wakipongezana baada ya kuangusha “mbuyu”
Huu unakuwa ni ushindi wa 10 wa Arsenal msimu huu na hivyo baada ya kutimiza alama 36, wamepanda hadi kwenye nafasi ya tano na tofauti kati yao na Manchester United walioko kwenye nafasi ya nne, ni alama moja pekee.
Katika mchezo huo, kocha Arsene Wenger alishuhudia mchezaji wake Matthieu Debuchy akitolewa nje kwa Machela baada ya kuteguka bega wakati akigombea mpira na mchezaji wa Stoke City, Marko Arnautovic.
Katika hali ya kawaida wakati kama huu ligi ya EPL hujigawa katika makundi matatu. Chelsea ambao wana alama 49 na Manchester City wenye alama 47, wanaonekana kupewa nafasi kubwa ya mmoja kuibuka na ubingwa na hili ni kundi la kwanza.
Kundi la pili ni lile linalowajumuisha Manchester United, Liverpool, Arsenal, Tottenham, Southampton na West Ham United ambao wanapigania kumaliza kwenye moja kati ya nafasi nne za juu ili kupata ushiriki wa Michuano ya Uefa msimu ujao.
Na kundi la mwisho, ni wale ambao wanapambana kukwepa kushuka daraja. Katika vita hii unakutana na timu kama Leicester City, Burnley, Crystal Palace, West Brom na hata QPR.
Msisimko kama huu ndiyo unaifanya ligi ya England kutotabirika kwani kila mchezo unakuwa na umuhimu kwa pande zote