*Maamuzi pia yalichangia*
Arsenal wameendelea kuwatibu washabiki wao, kwa kukubali kupoteza uongozi wa bao moja waliokuwa nao dhidi ya timu ndogo ya Watford, hata kama wamekuwa wakiwababaisha.
Washika Bunduki wa London walikuwa wakiongoza 1-0 hadi dakika ya 71 walipoadhibiwa kwa penati na kisha dakika ya 92 wakafungwa bao la pili na kuwapokonya hata pointi moja waliyokuwa wametarajia kurudi nayo London Kaskazini.
Kocha wa Arsenal, na baadhi ya wachezaji, wanawalalamikia waamuzi wakidai kwamba wamepoteza mechi kwa sababu ya wapinzani wao kupewa penati ambayo haikuwa sahihi; lakini ukifikiria zaidi, kwa nini hawakufunga mabao zaidi ili waondoke na ushindi hata kama penati ingetolewa?
Kwa nini waliruhusu yaliyotokea kufanywa na mchezaji au wachezaji wao? Kwa nini hawakuwashikilia vijana hao wa Watford kwenye nusu yao, ikijulikana kwamba Arsenal ni wenye uzoefu mkubwa uwanjani? Walipewa fursa za kutosha kusogea mbele na kufunga lakini hawakuonekana kupenda kufanya hivyo.
Na leo wakija watu wakasema kuna tatizo la DNA katika usakaji, usajili, upangaji na uchezaji wa wchezaji wa klabu hii, mwingine ataona kwamba huyo karopoka bila kutafakari, lakini ukweli ni kwamba kupoteza pointi rahisi kama hizi na mara kwa mara ndivyo hudunduliza na kufanya fungu la kukosa kwa jamaa hawa wa London Kaskazini mwaka hata mwaka.
Ilikuwa ni mechi ya mwisho ya Jumamosi, wenyewe bila shaka wakijua kwamba baadhi ya klabu za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL) zilikuwa zimewafanyia ‘wema’ kwa ama kwenda sare au kufungwa na yao mwishoni ingekuwa kazi rahisi kujihakikishia ushindi wa aina yoyote ili wachupe kwenye moja ya nafasi nne za juu.
Baada ya Liverpool na Manchester United kwenda suluhu, Crystal Palace kuwafunga Chelsea na Tottenham Hotspur kupata ushindi mwembamba wa 1-0 Arsenal wangechupa hadi nafasi ya nne.
Lakini pia matokeo mengine yalikuwa kwamba Burnley walitoshana nguvu ya 1-1 na West Ham, Man City akaachia mafuriko ya 7-2 kwa Stoke na Swansea akampiga Huddersfield, Arsenal ilikuwa waende kama kumsukuma mlevi tu.
Matokeo yake sasa Watford wapo nafasi ya nne, Arsenal wameporomoka hadi ya sita wakiwa na pointi 13 zile zile chini ya Chelsea wanaotoshana nao pointi sawa na Burnley na Liverpool. Wameaibisha.
Kule juu wamewaacha Manchester City wenye pointi 22, Man United 20, Spurs 17 na Watford 15. Wenger anadai kwamba mchezaji wa Watford, Richardson alijirusha, akajidai kwamba kaangushwa na beki wa pembeni wa Arsenal, Hector Bellerin na mwamuzi, Neil Swarbrick, akatoa penati.
Wachezaji wengi wa Arsenal walionekana kama vile hawakuwa vyema uwanjani; hawakujituma na naweza kusema kwamba ni nahodha Per Mertesacker angeweza kutoka uwanjani akiwa kifua mbele kwa jinsi alivyojituma, akadhibiti washambuliaji pale nyuma lakini pia akafunga bao kwa timu hiyo kipindi cha kwanza.
Haikuwa mbaya kumtoa Danny Welbeck na kumwingiza Mesut Ozil dakika ya 61 kwa sababu Mwingereza huyo aliumia kwa mara nyingine na Mjerumani akadhihirisha uwezo wake na kama si kukosa bao kwa Alez Iwobi alipopewa pasi nzuri na Ozil, si ajabu ushindi kwa Arsenal ungekuwa dhahiri.
Iwobi alirejea na kumpa mpira mwingine Ozil ambaye safari hii alitakiwa afunge lakini umaliziaji wake ukawa hovyo, akabaki kama asemwavyo mara kwa mara kwamba ni mwoga, anashindwa kutia juhudi zote za mwili na akili yake.
Wenger alimwondoa Alexandre Lacazette na kumwingiza Mfaransa mwenzao, Olivier Giroud kabla tu ya penati ile, lakini hata kama Lazacette hakuwa amefanya makubwa ingekuwa bora abaki angeweza kuwa na wakati wake, kwani ingemchukua muda Giroud kuuzoea mchezo na ndivyo ilivyokuwa, haikusaidia kitu.
Mara Arsenal wakawa chini ya shinikizo, Watford wakawatisha na kuwagawanya vipande vipande na kucheza walivyotaka. Arsenal walionekana kuchanganyikiwa, wakiangaliana badala ya kucheza mpira na kwenda nao mbele kufunga. Walikuwa wamefika mwisho wa kufikiri – hakuna tena zaidi ya pale.
Hakuna mwingine aliyeonekana kuwajibika kuhakikisha wanajimudu, kulinda lango kuhakikisha hawapotezi hata hako kapointi kamoja wakawa wanapelekeshwa tu kama bendera na upepo wake, matokeo yake bao la pili likaja mwisho kabisa wa mchezo na hiyo ni aibu kwa kocha na wachezaji wake kadhalika.
Arsenal wana matatizo, wanatakiwa kuyamaliza mapema iwezekanavyo vinginevyo wataishia wataishia pabaya. Kama ni gari, hawajafunga mkanda na uendeshaji si mzuri, hivyo cha kutokea wanatakiwa wawe wameshajua iwapo hawabadiliki.