*Chelsea, Man City, Man U kicheko
Wakati Arsenal wakivuna karamu ya mabao dhidi ya Sunderland, Chelsea wameendelea kushika uongozi wa Ligi Kuu ya England.
Baada ya kubanwa na Everton kwa zaidi ya dakika 90 kwenye dimba lao la Stamford Bridge, Chelsea walipata bao dakika za majeruhi baada ya mpira wa adhabu aliyofanyiwa Mbrazili Ramires.
Garry Cahil alitia kimiani mpira wa adhabu uliopigwa na Frank Lampard na kuwachosha kabisa vijana wa Roberto Martinez ambao kwenye mechi ya kwanza Goodison Park waliwapiga The Blues.
ARSENAL WATULIZA AKILI, WASHINDA
Upande wa kaskazini mwa London, vijana wa Arsene Wenger wenyewe walicheza gemu linaloitwa kwamba ndilo hasa la Arsenal, na kuwazidi nguvu Sunderland kwa 4-1.
Hadi mapumziko Arsenal walikuwa mbele kwa 3-0 kwa mabao mawili ya kuongoza ya Olivier Giroud kabla ya jingine zuri la Tomas Rosiscky na la kumalizia kwa kichwa la beki wa kati, Laurent Konscielny.
Sunderland walifuta machozi kwa bao la baadaye la Emanuele Giaccherini na kumaliza mfululizo wa mechi tano za Arsenal za EPL bila kufungwa bao Emirates.
STOKE WABANA, KISHA WAACHIA MAN CITY
Manchester City nao walipata tabu mbele ya Stoke City inayogangamala vilivyo siku hizi chini ya kocha Mark Hughes, lakini waliachia baadaye kwa kuruhusu bao la Yaya Toure na kutoka 1-0.
Kwa matokeo hayo, Chelsea wameendelea kuongoza kwa kufikisha pointi 60 wakifuatiwa na Arsenal wenye 59 na Man City 57 lakini vijana hao wa Manuel Pellegrini wana mchezo mmoja mkononi.
MANCHESTER UNITED WAPATA USHINDI
Baada ya kufanikiwa kumshawishi Wayne Rooney kusaini mkataba mwingine wa miaka mitano, Manchester United walicheza na Crystal Palace na kushinda 2-0.
Manchester United wamemaliza mechi tatu mfululizo za ligi pasipo ushindi, ambapo walipata mabao yao kwa penati ya Robin van Persie dakika ya 62 na Wayne Rooney akafunga dakika sita baadaye.
RVP alifunga penati baada ya Patrice Evra kuchezewa faulo na Marouane Chamakh.
MATOKEO MENGINE YA EPL
Katika mechi nyingine, kwa mara ya kwanza Hull City walipata ushindi mnono EPL ambapo waliwaadhibu Cardiff 4-0.
West Bromwich Albion wakicheza nyumbani walikwenda sare ya 1-1 na Fulham wakati West Ham United wamejiweka pazuri kwa kushinda mfululizo, safari hii wakiwapiga Southampton 3-1.
Nafasi tatu za mkiani zinashikiliwa na Sunderland wenye pointi 24, Cardiff 22 na Fulham 21 lakini Sunderland wana mchezo mmoja mkononi.