*Wawachapa Bayern kwao, lakini waaga UCL
*Malaga, Barca na Galatasaray robo fainali
Arsenal wametoka nje ya michuano ya Kombe la Mabingwa Ulaya (UCL) kwa heshima, baada ya kuwafunga Bayern Munich mabao 2-0.
Kocha Arsene Wenger alifanya mabadiliko makubwa kwa kikosi kilichoanza, akimweka kando golikipa Wojciech Szczęsny, nahodha Thomas Vermaelen na kukosekana nyota wengine kama Jack Wilshere na Lukas Podolski.
Katika mechi ambayo wengi walitarajia Arsenal kufungwa mabao mengi baada ya kuchapwa 3-1 Emirates kwenye mechi ya kwanza, walisawazisha makosa yote.
Washika Bunduki hao wa London wametoka nguvu sawa na Bayern kwa jumla ya mabao 3-3, lakini Bayern wamesonga mbele kwa faida ya goli moja ya ugenini.
Golini alikaa Lukasz Fabianski ambaye hakuwa amecheza kwa zaidi ya mwaka mmoja, huku Kieran Gibbs akirejea kutoka majeruhi, na walikuwa Olivier Giroud na Laurent Koscienly waliofunga mabao kwa The Gunners.
Wachambuzi wanasema Arsenal wamerejesha heshima na hata kama hawapati kombe msimu huu, wakichukua mazuri ya mchezo huo, wanaweza kumaliza vizuri Ligi Kuu ya England (EPL) wanakorejea sasa kupigania nafasi ya tatu au ya nne.
Tofauti na mechi zilizotangulia za mashindano tofauti, Arsenal walionesha uimara mkubwa kwenye beki yake, hsa Koscienly na Per Mertesacker.
Maana ya matokeo hayo ni kwamba Uingereza haitakuwa na timu yoyote kwenye hatua ya robo fainali.
Katika mechi nyingine Malaga kutoka Hispania wamevuka hadi hatua ya robo fainali, baada ya kuwashinda Porto wa Ureno mabao 2-0, baada ya kulala bao 1-0 katika mechi ya awali.
Jumanne Barcelona iliweka historia kwa kuwatoa AC Milan kwa mabao 4-0, baada ya kuwa wamefungwa mabao 2-0 katika mechi ya awali nchini Italia.
Barca walirejesha heshima yao iliyopotea wiki kadhaa zilizopita kwa kufungwa mara mbili na Real Madrid kwenye mechi za Hispania na kichapo hicho cha Milan.
Mabao ya Barca yalifungwa na Lionel Messi mawili, David Villa na Jordi Alba. Barca ndiyo timu ya kwanza kugeuzia kibao timu iliyowafunga kabla bila kutegemea bao la ugenini.
Kwa ushindi huo, Barcelona wamefikisha mechi 20 bila kufungwa kwenye uwanja wao wa Nou Camp.
Katika mechi nyingine, Galatasaray waliwatoa kwenye mashindano Schalke kwa mabao 3-2 katika mchezo uliochezwa nchini Ujerumani, baada ya kuwa wametoka sare ya bao 1-1 kwenye mechi ya awali Uturuki.
Timu zilizoingia robo fainali ni Barcelona, Bayern Munich, Borrusia Dortmund, Galatasaray, Juventus, Malaga, Paris Saint Germain na Real Madrid.