*Swansea wawazuia Southampton
Arsenal wameonesha soka ya kuvutia baada ya baadhi ya nyota wake kurejea kutoka kwenye mapumziku ya matibabu, huku chipukizi Hector Bellerin na Chuba Akpom nao wakionesha makali kwenye ushindi wa 5-0 dhidi ya Aston Villa.
Washika Bunduki wa London walicheza nyumbani Emirates, lakini wakikabiliana na timu yenye uzoefu wa kuwafunga kwenye uwanja wao wa nyumbani, hivyo Kocha Arsene Wenger akawaonya mapema kwamba wawe makini.
Mabao ya wenyeji yalifungwa na Mesut Ozil, Theo Walcott, Olivier Giroud, Santi Cazorla na Bellerin, golini mwa Arsenal akianza tena kipa David Ospina huku Danny Welbeck na Alexis Sanchez wakiwa nje kutokana na majeraha tofauti.
Hii ni mara ya kwanza kwa Arsenal kufunga mabao matano kwenye mechi moja msimu huu na ushindi umekuwa wa tatu mfululizo, ambapo kati ya pointi 24 walizokuwa wakitafuta wamechuma 19, wakipambana kutafuta kuingia kwenye nne bora.
Katika matokeo mengine, Swansea wamefanikiwa kuwafunga sounthampton 1-0 na kuwapunguza kasi yao, bao likifungwa na Jonjo Shelvey katika dakika ya 83, ukiwa ni ushindi wao wa kwanza hapo St Mary’s katika miaka 62.
Kwa matokeo hayo na ya Jumamosi Chelsea wanashika usukani bado kwa pointi 53, wakifuatiwa na Manchester City wenye 48, Manchester United waliofikisha 43, Southampton na Arsenal wanazo 42 huku Spurs wakiwa nazo 40.