*Hawawezi kusajili kama Jose Mourinho
*Chelsea, Man City, Man U noti nje nje
*Arsenal wakiwaiga watashuka daraja
KWA hali ya hewa ya soka ilivyo, nawaona Arsenal wakibaki walipo au
kurudi nyuma kutokana na klabu nyingine zilivyodhamiria, lakini pia
kufanya kweli kusajili majina makubwa.
Arsenal wamebaki tu katika matumaini kwamba Arsene Wenger atafanya
kitu kabla ya dirisha kufungwa baada ya kama wiki mbili hivi na ushee.
Utasikia klabu nyingine wakijitapa kwamba wanataka mchezaji kama Paul
Pogba au James Rodriguez, au Gonzalo Higuain, au Angel Di Maria au
Zlatan Ibrahimovic aur Raheem Sterling au Neymar na kuna
waliofanikisha ndoto hizo kwa vitendo.
Wapo wanaosema kwamba Arsenal wangeweza kusajili aina ya vigogo kama
hao au hata kuandika hawala ya fedha kama aliyoamua Jose Mourinho wa
Manchester United iandikwe ili kuingiza wachezaji nyota Old Trafford.
Naam, kuna wanahabari wanadhani kwamba Arsenal wanaweza kuandika
hawala ya fedha kama ya wenzao wa Real Madrid, Chelsea, Manchester
City, au Barcelona waliyoandika kwa ajili ya kununua wachezaji wapya.
Lakini kuna mahali tunakosea; kwa sababu kiukweli ni kwamba Arsenal
hawawezi kumudu mambo makubwa haya au labda tuseme hakuna mpango wa
matumizi makubwa kihivyo.
Pauni milioni 89 ni ada ya uhamisho tu, lazima upige hesabu ya
mishahara vile vile. Hununui mtu kwa bei mbaya ukaja kuishia kumlipa
mshahara sawa na pesa ya mboga au ya ugoro.
Fikiria, mshahara wa Pogba ni £290,000 kwa wiki, yaani karibu pauni
milioni 15 kwa mwaka.
Gharama kubwa kwa Ibrahimovic, ambaye kama Pogba wapo Manchester
United haikuwa ada bali mashahara wa pauni 260,000 kwa wiki,
utakaofika pauni milioni 12.4 kwa mwaka.
Hatujamaliza; njoo kwa Henrikh Mkhitaryan aliyenunuliwa kwa ada ya
pauni milioni 35.7 na mashahara wake kwa wiki ni pauni 200,000 (pauni
milioni 10.4 kwa mwaka).
Kuna mtu anaitwa Eric Bailly ambaye ada ya uhamisho ilikuwa pauni
milioni 32.3 na mashahara wake kwa wiki unakuwa £75,000 (pauni milioni
3.9 kwa mwaka).
Sasa, hizi ni kwa wachezaji wanne na utaona kwamba gharama ni pauni
milioni 42.7 kwenye mishahara wakati ada ya uhamisho iliyotumika kwao
ni pauni milioni 155. Hiyo ni gharama ya pauni milioni 197.7 kwa
wachezaji wanne, na ni vyema kuelewa kwamba wachezaji wanne hawatoshi
kwa kikosi cha timu.
Ni ngumu kuja na takwimu za gharama za mishahara ya wachezaji. Kwa
mfano, Mkhitaryan ana mshahara wa awali, kwa mujibu wa vyanzo fulani,
wa £140,000 huku zikiwekwa hapo nyongeza nyingine ambazo ni rahisi
kwake kufuzu kuzipata kiasi cha kufikisha mshahara wake kufika
£200,000 kwa wiki, lakini ni mzigo mzito kwa klabu.
Kwa hiyo, wachezaji hao wanne hali ni hiyo. Hili linaonekana kwa mmoja
wa wachambuzi wa soka kuwa Arsenal wanahitaji. Mabeki wawili wa kati,
mshambuliaji wa kati mmoja na winga mmoja.
Kwa mujibu wa mahitaji ya timu, Laurent Koscielny anahitaji kuwa na
mtu mwingine lakini pia anatakiwa mshambuliaji wa kiwango kikubwa
kimataifa kuchukua nafasi ya Olivier Giroud na mwingine kuchukua
nafasi ta Theo Walcott.
Mapendekezo ni kwamba Arsenal walitakiwa na lazima wasaini kitu
kilichokamilika; wachezaji wa kiwango kikubwa kabisa kimataifa walio
katika kilele cha mafanikio yao kisoka.
Kwamba Arsenal wanaweza kumudu kuwapata lakini ukweli ni kwamba
hawawezi, ikiwa wanataka kubaki kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) walau
kwa misimu mitatu kuanzia sasa.
Arsenal hawana fedha inayotakiwa kununua na kuwalipa wachezaji wa aina
hiyo na kwa bei hizo za juu na mishahara walipwe mwaka hata mwaka.
Man United wanaweza. Chelsea wanamudu kwa kukwepa kunaswa na kanuni na
kugharamia wachezaji kutoka mfukoni mwa mmiliki wao.
Manchester City nao wanafanya hivyo hivyo na haya yanachukuliwa na
baadhi ya watu kwamba ni habari nzuri namafanikio kwao; labda ndivyo
ilivyo, lakini si endelevu. Ukitaka kujua bepari anafanya nini
anapochoka na mwanasesere wake, waangalie Aston Villa.
Villa ni klabu waliokuwa karibu juu ya soka ya England kwa zadi ya
karne moja. Walitwaa makombe zama za kabla ya EPL na uwekezaji wa
Randy Learner uliwavuta karibu na kuelekea kutwaa ubingwa mara kadhaa.
Hakufanikiwa kuupata hata mara moja lakini.
Baada ya hapo aliboreka; yaani akachokana na timu hiyo kama kabaila
anavyochokana na mwanasesere wake.
Man City, Man United, Chelsea na Arsenal walikuwa wakubwa zaidi ya
Villa na walitumia fedha zaidi. Learner aliamua kuacha kuwekeza fedha
zake kwenye klabu yenye historia kubwa na washabiki wengi na leo hii
wametumbukia Ligi Daraja la Kwanza (Championship).
Hiyo inaweza kutokea. Iwapo Arsenal watatumia fedha kama hizo na kwa
bahati mbaya wakaenda mwelekeo mbaya, uwezekano uliopi ni mkubwa
kwamba wanaweza kuelekezwa walikoishia Villa au Newcastle au Blackburn
au Portsmouth.
Uthabiti ule ule unaowahakikishia Arsenal wanapambana na kuwania hasa
ubingwa mwaka hadi mwaka hautakuwapo ikiwa Arsenal watatumia fedha
kijinga. Wakitoa pauni milioni 89 kwa ada ya mchezaji aliye kiwango
sawa na viungo Javier Martinez, Blaise Matuidi, Luca Modric, na Arturo
Vidal utakuwa ni upuuzi.
Lakini kwa United yaweza ikawa si upuuzi kwani wanamudu na wanaweza
kufanya kosa la pauni milioni 89 lakini kwa Arsenal hapana, itakuwa ni
kujiua. Na si kwamba eto Mourinho huwa hakosei, anakosea sana.
Wako wapi na wamefanya nini akina Mohamed Salah, Juan Cuadrado, Abdul
Rahman Baba, Papy Djilobodji, Falcao, Andre Schurrle, Marco van Ginkel
na Filipe Luis?
Hawa ni wachezaji aliowasajili Chelsea na kwa hali ilivyo sasa badala
ya kuwa The Only One, The Special One, The Happy One anakuwa The
Spending One (Mzee wa Matumizi kama Kasimu aliyekuja kufilisika baada
ya kununulia mabibi bia kwa wingi akitoa ofa). Wachezaji wake hao
wamekuja kumgeukia magarasa Stamford Bridge.
Kwa maeneo machache klabu ilijirejeshea fedha zao lakini wachezaji
walishindwa. Mourinho pia alifanya makosa kwa kumwondisha Romelu
Lukaku aliyedhaniwa angetokea kuwa Didier Drogba mpya.
Sasa makocha wote wanafanya makosa, lakini gharama za makosa
zinatofautiana. Unapozungumzia makosa ya mamia ya mamilioni ni tofauti
kwa klabu moja na nyingine, wakati baadhi zinaweza kufa nyingine
ambazo waleti zao za fedha hazikauki kama Chelsea, Man City au Man U
wanamudu hayo.
Arsenal wanaweza kuwa wanashindana na timu nyingine za EPL uwanjani,
lakini inapokuja kwenye usajili wa wachezaji wapya wanashindana na
klabu kubwa kote duniani.
Juventus walimuuza Pogba na kumnunua Gonzalo Higuain. Bayern Munich,
Real Madrid, Barcelona na PSG wote wana mifuko mikubwa kuliko Arsenal.
Kwa kuachwa nyuma huku, habari hii hii imekuwa ikielezwa kila mwaka
wakati kama huu na vichwa vya habari vikisema vitu kama; Arsenal
wapitwa tena fedha za usajili, Arsenal katika hatari ya kuachwa nyuma,
Arsenal hawawezi kushindana.
Huu ni mwaka ambao wangeweza kuanguka kutoka timu nne bora kwenye
msimamo wa ligi kuu. Inaweza ktokea, kweli kabisa. Timu sita juu
kwenye msimamo ni kali sana.
Tottenham Hotspur watakuwa wazuri, Man United watajiimarisha, ikiwa
Mourinho atawapeleka vyema; Man City watakuwa wazuri; sioni Chelsea
wakiwa wabaya na Liverpool …hawaelekei kufanya kazi vya kutosha kuweza
kuwa kwenye tano bora.
Wachezaji walionunua wanafanana na wale Brendan Rodgers aliowanunua;
wazuri lakini si wa kiwango kikubwa kabisa kimataifa. Kocha wa
Liverpool, Jurgen Klopp ni mzuri kwa nafasi yake hata hivyo, na huenda
akamudu kuishikilia.