Menu
in , , , ,

Arsenal hapatoshi Wembley leo

 

*Fainali ya FA dhidi ya Hull City

Arsenal wanajaribu kumaliza ukame wa miaka minane na ushee wanapojitupa Uwanja wa Wembley kwenye fainali ya Kombe la FA.

Vijana hao wa Arsene Wenger watachuana na Hull City – timu iliyopanda daraja msimu uliomalizika majuzi na kufanikiwa kubaki Ligi Kuu ya England (EPL).

Wenger amekuwa kwenye shinikizo la kutwaa vikombe na ni moja ya sababu za baadhi ya wachezaji wake nyota kuondoka, wa karibuni zaidi akiwa ni Robin van Persie aliyejiunga Manchester United.

Hata hivyo kuanzia msimu uliopita Arsenal walianza kutumia fedha nyingi kuimarisha kikosi chao, ikiwa ni pamoja na kuvunja rekodi ya klabu kwa kumnunua Mesut Ozil kutoka Real Madrid kwa zaidi ya pauni milioni 40.

Arsenal waliofanikiwa kumaliza ligi wakiwa nafasi ya nne baada ya ushindani mkubwa kutoka kwa Everton na kidogo kutoka kwa jirani zao wa London Kaskazini – Tottenham Hotspur watatakiwa kuwa makini hata kama Hull wanaofundishwa na Steve Bruce si timu ya kutisha, wanaweza kuwaaibisha.

Ilikuwa ni 2005 katika mechi ya Kombe la FA pia ambapo Arsenal walitwaa taji kwa mara ya mwisho mikononi mwa Manchester United katika Uwanja wa Cardiff.

Kocha Bruce amekiri kwamba timu yake haipewi nafasi kubwa kutwaa kombe hilo kutokana uzoefu wa Wenger na klabu yake ambao wametwaa makombe saba makubwa hadi sasa.

“Arsenal wanapewa nafasi kubwa na ya wazi lakini kwa klabu kama yetu kukabiliana nao dimbani kwenye fainali ni jambo kubwa,” alisema Bruce.

Mechi hiyo itakayopigwa jioni ya saa moja kwa saa za Afrika Mashariki inatarajiwa kuhudhuriwa na washabiki wanaokaribia 90,000.

Wenger alichelewesha mazungumzo juu ya kuhuisha mkataba wake kuendelea kuwanoa Washika Bunduki wa London msimu ujao baada ya kuanza kuteleza kwenye ligi kuu, lakini baada ya kujihakikishia ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwakani, amesema atabaki Arsenal hata wasipotwaa Kombe la FA.

Anasema ukame wa makombe umefanya mambo kuwa magumu na anasisitiza kwamba hawatakiwi kucheza kwa historia bali kwa kuzingatia kiwango cha sasa.

Msimu wa soka unamalizika Ulaya kwa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya Real Madrid na Atletico Madrid Jumamosi ijayo kabla ya kupisha fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil kuanzia Juni 12.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version