*Spurs mdomoni mwa Dinamo Tbilisi tena
*Watuhumiwa wa upangaji matokeo ndani
Miamba wa London Kaskazini, Arsenal watachuana na Fenerbahce ya Uturuki katika mchujo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Washika Bunduki hao walioshika nafasi ya nne Ligi Kuu ya England watalazimika kupata uwiano mzuri wa matokeo kuliko Waturuki hao, ili wapate nafasi miongoni mwa klabu 32 zitakazocheza kwenye hatua ya makundi.
Fenerbahce wamefutiwa adhabu ya kukosa mashindano ya Ulaya kwa miaka miwili waliyokuwa wamepewa Juni, baada ya kutiwa hatiani kwa kupanga matokeo.
Wameruhusiwa kuendelea na mechi kutokana na kukata rufaa, ambapo rufaa yao itasikilizwa mwezi huu, na mechi ya awali ikiwa Uturuki Agosti 21 na marudio Emirates, London siku sita baadaye.
Fenerbahce walikata rufaa kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), baada ya wao na
Besiktas kuadhibiwa na Uefa, ambapo CAS inatarajia kutoa uamuzi kabla au ifikapo Agosti 28, siku inayoweza kuwa ya mechi ya marudiano na Arsenal.
Uefa wanasema hawajaamua kipi kitafanyika iwapo Fenerbahce watashinda na kufuzu, na kisha kupoteza rufaa yao.
Timu mbili hizo zilikutana katika mashindano hayo katika Kundi G msimu wa 2008/2009, Arsenal wakashinda mabao 5-2 nchini Uturuki, kisha wakatoa suluhu nyumbani Emirates kwenye marudiano.
Klabu ya Ukraine, Metalist Kharkiv, ambao wamepangwa dhidi ya Schalke ya Ujerumani kwenye Ligi ya Mabingwa, nao wanasubiri kusikilizwa kwa shauri lao la kinidhamu na Uefa wiki ijayo, baada ya kushindwa rufaa kuhusu upangaji matokeo mwaka 2008.
Celtic ya Uskochi itasafiri hadi Kazakhstan kuchuana na Shakhter Karagandy kwenye mechi ya awali.
Tottenham Hotspur wataanza mchujo wa Ligi ya Europa nchini Georgia watakapokabiliana na Dinamo Tbilisi.
Spurs wanaofundishwa na Mreno Andre Villas-Boas walipoteza mechi ya robo fainali kwenye mikwaju ya penati dhidi ya Basel ya Uswisi msimu uliopita, na walikutana na Tbilisi kwenye Kombe la Uefa mwaka 1973, wakashinda 1-1 ugenini kabla ya kuwatandika 5-1 nyumbani London.
Mabingwa wa Kombe la Ligi la England, Swansea wamerejea kwenye mashindano ya Ulaya kwa mara ya kwanza tangu 1991, baada ya kuvuka mchujo walipowafunga Malmo 4-0, watacheza dhidi ya Petrolul Ploiesti ya Romania.
Mechi za kufuzu zitachezwa kati ya Agosti 22 na 29, ambapo droo ya hatua za makundi inatarajiwa kutolewa Agosti 30, ikihusisha Mabingwa Kombe la wa FA wa England, Wigan, ambao pia walishuka daraja mwaka jana.
Mabingwa mara saba AC Milan wamepangwa na Mabingwa wa Ulaya wa mwaka 1988, PSV Eindhoven, huku Wafaransa Lyon wakikutana na Real Sociedad kutoka Hispania.