Mabao matatu yaliyotiwa kimiani na Andy Carroll dhidi ya Arsenal
yamewatibulia Arsenal ndoto za ubingwa, baada ya kwenda sare ya 3-3 na
West Ham.
Kwa matokeo hayo, Arsenal wenye pointi 59 wanakuwa pointi 10 nyuma ya
vinara Leicester na pointi tatu nyuma ya Tottenham Hotspur, zikiwa
zimebaki mechi sita kumalizika kwa msimu.
Mesut Ozil na Alexis Sanchez walizitendea haki pasi za chipukizi Alex
Iwobi na kuwafanya Arsenal kuwa mbele kwa mabao 2-0 lakini Carroll
akafunga mabao mawili ndani ya sekunde 160 na kusawazisha mambo hadi
nusu ya kwanza ya mchezo inamalizika.
Carroll tena alifunga kwa kichwa na kukamilisha hat-trick yake lakini
beki wa kati Mfaransa Laurent Koscielny alisawazisha akiwa umbali wa
yadi 10.
Wenyeji West Ham waliendeleza rekodi ya kutofungwa nyumbani hadi mechi
14, lakini vijana hao wa Slaven Bilic wanabaki katika nafasi ya sita,
pointi mbili nyuma ya Manchester City.
Vijana wa Manuel Pellegrini walifanikiwa kutoka na ushindi wa mabao
2-1 dhidi ya West Bromwich Albion na kubaki nafasi ya nne.
Manao ya City yalifungwa kwa penati ya Sergio Aguero na Samir Nasri
aliyerejea kutoka kwenye majeruhi. Bao la West Brom lilifungwa na
Stephane Sessegnon mapema dakika ya sita.
Sessegnon alivuruga kazi yake nzuri kwa kumwangusha Aleksandar Kolarov
kwenye eneo la penati ndipo Aguero akafunga.
Matokeo mengine Jumamosi hii ni Crystal Palace kuwafunga Norwich 1-0,
Aston Villa wakalala nyumbani kwa 1-2 dhidi ya Bournemouth.
Southampton waliendeleza balaa dhidi ya Newcastle kwa kuwakung’uta
mabao 3-1, Swansea wakawapiga Chelsea 1-0 na Watford wakatoshana nguvu
na Everton kwa 1-1.