*Arsenal wajipa matumaini*
Arsenal na Chelsea wamefanya vyema kwenye mechi zao za Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), baada ya kupata ushindi mnono dhidi ya wapinzani wao.
Wakicheza nyumbani, Arsenal waliwatandika Dinamo Zagreb 3-0 na sasa watahitaji ushindi mwingine mkubwa watakaposafiri kwenda kucheza na Olympiakos kwenye mechi ya mwisho.
Walifarijika pia kwa sababu walihitaji Bayern wawafunge Olympiakos Jumanne hii, jukumu ambalo vijana wa Pep Guardiola walitimiza.
Mchezaji bora wa mechi ya Jumanne hii, Mesut Ozil ndiye alifungua kitabu cha mabao kabla ya ‘mkombozi’ Alexis Sanchez kufunga mawili.
Arsenal walianza vibaya mashindano haya kwa kupoteza mechi mbili dhidi ya Zagreb na Olympiakos, kabla ya kuwafunga Bayern ambao hata hivyo walijibu mapigo kwenye mechi ya marudiano.
CHELSEA WAWAPIGA MACABI 4-0
Chelsea wamewafunga Maccabi Tel Aviv 4-0 na kusonga hadi nafasi mwenza ya kwanza katika kundi lao la G.
Mabao yao yalitiwa kimiani na Gary Cahill, Willian, Oscar na Kurt Zouma. Porto waliokuwa wakiongoza walifungwa na Dynamo Kiev, hivyo sasa Chelsea wanahitaji pointi moja tu kufika hatua ya mtoano.
Katika mechi nyingine, Barcelona wakicheza nyumbani waliwachakaza Roma 6-1, Bayern Munich wakawapiga Olympiakos 4-0, BATE Bor wakaenda sare ya 1-1 na Bayer Leverkusen, Zenit St Petersburg wakashinda 2-0 mbele ya Valencia na Lyon wakalala 1-2 kwa KAA Gent.