Menu
in , , ,

Argentina, Ujerumani hapatoshi

MWALI anatolewa Jumapili hii katika fainali ya michuano ya Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.

Piga ua, lazima mshindi apatikane kwenye mechi baina ya Argentina na Ujerumani waliofanikiwa kuvuka vigingi vyote, japo wakati mwingine kwa jasho la damu hadi kufikia mechi hii ya 64 na ya mwisho ya fainali hizi.

Argentina wanaingia fainali baada ya mechi ya mwisho kuwashinda kwa mikwaju ya penati Uholanzi wakati Ujerumani wanaingia kwa ushindi mchekea wa mabao 7-1 dhidi ya wenyeji Brazil.

Ujerumani wanaweza kutaja na kuanza na kikosi kile kile kilichowaangamiza Brazil ili kuweka msisitizo kwa maana wote wapo fiti kiafya na kwa kiwango wakati kwa Argentina bado hakuna uhakika iwapo Angel Di Maria aliyeumia kwenye mechi ya robo fainali na kukosa nusu fainali atacheza.

Striker Sergio Aguero wa Argentina ameshakuwa fiti kabisa na anaweza kuanza badala ya ama Ezequiel Lavezzi au Gonzalo Higuain. Argentina wamepata kuwachezesha Higuain, Aguero na Lionel Messi kama washambuliaji kwenye nafasi ya mbele siku zilizopita.
Argentina

Hata hivyo, kutokana na hali nzuri ya Ujerumani, kuna uwezekano wa kocha Alejandro Sabela kuachana na mpangilio huo ili kuimarisha zaidi kiungo. Beki wa kushoto, Marcos Rojo naye alikuwa na matatizo ya mkono Ijumaa, haijajulikana kama atacheza.

Hii ni mechi ya tatu ya fainali inayokutanisha timu hizi, ikiwa ni pamoja na iliyokuwa Ujerumani Magharibi. Mwaka 1986 Argentina waliwapepeta Ujerumani Magharibi 3-2 lakini wakaja kufungwa 1-0 mwaka 1990
Ni mara moja tu Argentina wamewashinda Ujerumani katika mechi nyingine za Kombe la Dunia ambapo 2006 na 2010 Ujerumani ndio waliwatoa Argentina katika hatua za kabla ya fainali.

Hii ni mara ya nane kwa Ujerumani kufika fainali ya michuano hii mikubwa, ikiwa ni rekodi mpya inawekwa, ambapo wameshinda mara tatu na kupoteza nne. Ikiwa watashinda Jumapili hii watakuwa sawa na Italia ambao hadi sasa wameshalitwaa kombe hilo mara nne.

Ushindi pia utawafanya Ujerumani kuwa taifa la kwanza la Ulaya kutwaa kombe hili katika ardhi ya Amerika. Ujerumani ndio wanashika rekodi ya kufungwa zaidi mechi ya fainali lakini pia wana rekodi ya kutoshindwa katika mechi zao 17 za kimataifa zilizopita, ambapo walishinda 12 na kwenda sare tano.

Kufungwa kwao mara ya mwisho ilikuwa dhidi ya Marekani kwa mabao 4-3 katika mechi ya kirafiki Juni mwaka jana. Sare ya mwisho ni dhidi ya Ghana katika hatua ya makundi mwaka huu.

Argentina, au kama wanavyojulikana La Albiceleste wamefanikiwa kutofungwa hata bao moja kwenye mechi nne za fainali hizi na bado hawajapata kufungwa bao katika hatua za mtoano. Lionel Messi ametengeneza nafasi 21 za kufunga kwenye michuano hii, zikiwa ni nyingi kuliko mchezaji mwingine yeyote.

Hata hivyo, Messi ambaye ndiye tegemeo la Argentina ameshindwa kufunga hata bao moja katika mechi tatu zilizopita za michuano hii lakini tangu Sabella aichukue timu Agosti 2011, Messi hajacheza mechi nne bila kufunga, hivyo Waargentina wanadhani atafunga Jumapili hii na kuwapa faraja.

Argentina wana wastani wa wachezaji wenye umri wa miaka 29 na iwapo watatwaa kombe hili watachukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Italia kwa kuwa ‘wazee’ zaidi waliochukua kombe hili. Hawajawahi pia kutangulia kufungwa bao katika michuano ya mwaka huu.

MWAMUZI WA MECHI

Mwamuzi wa mechi ya Jumapili hii ni Mtaliano, Nicola Rizzoli, ambapo jina la Mwingereza
Howard Webb lilipendekezwa pia kabla ya uamuzi wa mwisho kufanyika.
Mechi hii inafanyika katika Uwanja wa Maracana, Rio De Janeiro. Rizzoli (42) ni mtaalamu wa ramani za majengo anayetoka jijini Bologna na tayari amechezesha mechi tatuz a mashindano ya mwaka huu.

Ndiye alichezesha mechi baina ya Hispania na Uholanzi; Nigeria na Argentina na pia Argentina dhidi ya Ubelgiji, kwa hiyo Argentina wana uzoefu naye ikiwa uzoefu huo hupatikana kwa kucheza mechi anayochezesha, lakini kama ni vinginevyo, Wajerumani ndio watakuwa wamemsoma zaidi maana walikuwa wanamwangalia akichezesha wenzao labda.

Lakini Rizzoli alichezesha pia michuano ya Kombe la Europa 2010 hatua ya fainali baina ya Atletico Madrid ya Hispania na Fulham ya Uingereza na fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya Bayern Munich na Borussia Dortmund mwaka jana, timu zote zikiwa za Ujerumani na zilizotoa wachezaji wengi wa timu ya taifa.

Rizzoli atasaidiwa na waamuzi kutoka nchini mwake, Renato Faverani na Andrea Stefani, huku mwingine kutoka Ecuador, Carlos Vera akiwa mwamuzi namba nne. Rizzoli anakuwa Mwtaliano wa tatu kuchezesha fainali za Kombe la Dunia baada ya Sergio Gonella mwaka 1978 na Pierluigi Collina mwaka 2002.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version