Mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Manchester United ya Uingereza, Andy Cole, anatarajiwa kuwasili nchini leo kwa ajili ya kuzindua mpango maalum wa kuibua vipaji vya soka kwa vijana utakaosimamiwa na klabu hiyo bingwa ya England.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na kampuni ya Airtel, ambayo ndiyo iliyoandaa programu hiyo kwa nchi za Afrika ikienda kwa jina la “Nyota wa Soka Wanaoinukia wa Airtel”, kama sehemu ya udhamini wake wa miaka minne kwa klabu hiyo, Andy Cole atazindua mpango huo leo saa 4 asubuhi kwenye shule ya Sekondari ya Makongo.
Mpango huo utashirikisha vijana zaidi ya 500 wa umri wa chini ya miaka 17, ambao wataonyesha vipaji vyao katika michuano itakayoandaliwa kwa ngazi ya mikoa na taifa na kusimamiwa na makocha wa shule za soka za Manchester United.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, Leodgar Tenga, alisema kuhusu mpango huo ni jambo kubwa zaidi kupata kutokea katika soka la Tanzania.
“Mipango ya aina hii katika kuibua na kuendelea vipaji vya wanasoka chipukizi ni ufunguo katika kuinua soka la nchi. Na kinachofanya mpango huu wa ‘Nyota wa Soka wa Airtel’ kuwa ‘spesho’ ni ushirikiano wao na Manchester United, moja ya timu kubwa zaidi duniani. Hii inafanya kuwa moja ya mambo bora zaidi yaliyopata kutokea katika soka la Tanzania. Tunajivunia ushirikiano huu na tunaahidi kusapoti mpango huu”.
Akizungumzia sapoti yao katika mpango huo wa “Nyota wa Soka Wanaoinukia wa Airtel”, Mwenyekiti Mtendaji wa Manchester United, David Gill, alisema; “Tunayo furaha kuwasapoti Airtel katika mpango huu na tunawapongeza kwa kusaidia kuibua utajiri wa vipaji vya soka kwa vijana kupitia ‘Airtel Rising Stars’ katika masoko yao 12 barani Afrika. Makocha wa shule ya soka wa Manchester watawafundisha vijana hawa kucheza kwa namna ya Manchester United inavyocheza.”
Fomu za kujisajili kwa ajili ya mpango huo unaotarajiwa kushirikishia vijana zaidi ya 500, utafanyika hadi mwisho wa Julai mwaka huu na zitapatikana katika ofisi za Airtel kote nchini.
Cole aliyetwaa makombe matano kati ya 19 waliyonayo Man U ya Ligi Kuu ya England, aliichezea klabu hiyo kwa misimu 7. Jana alikuwepo nchini Kenya kwa shughuli kama hizo.