Menu
in , , ,

Andre Villas-Boas afukuzwa kazi

 

Tottenham Hotspur wamemfukuza kazi kocha wao, Andre Villas-Boas.

 

Hatua hiyo imekuja baada ya matokeo mabaya mwishoni mwa wiki, ambapo Spurs walifungwa 5-0 na Liverpool katika mechi ya Ligi Kuu ya England (EPL).

 

Kipigo hicho kilikuwa kikubwa zaidi kwa Spurs katika dimba la White Hart Lane katika miaka 16 na kiliwaacha wakiwa katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi, nyuma ya mahasimu wao wa London Kaskazini kwa pointi nane, Arsenal.

 

AVB aliitwa ofisini kwa Mwenyekiti, Daniel Levy usiku wa kuamkia Jumatatu hii baada ya kichapo na kufutwa kazi lakini wengi wanajiuliza iwapo kuna mbadala bora zaidi yake kwa sasa.

 

Baada ya mechi hiyo ambayo Liverpool haikuwa na nyota wake na ilitarajiwa kufungwa, AVB alionekana kupoteza matumaini, kutojiamini na kutafuta pa kujishikia, akisema bado kwenye Ligi ya Europa wamo na makombe mengine ya nyumbani.

 

Villas-Boas (36) aliyepata kuwafundisha Chelsea na kufukuzwa, alianza kazi yake ya sasa Julai 12 mwaka jana baada ya kufutwa kazi kwa kocha mwingine, Harry Redknapp licha ya kuifanya kazi yake vizuri.

 

Alishinda asilimia 53.7 ya mechi za ligi alizokuwa kiongozi, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi kwa kocha yeyote Spurs tangu kuanza kwa EPL 1992.

 

Hata hivyo, shinikizo dhidi ya AVB lilizidi baada ya kukung’utwa na Manchester City 6-0 Novemba 24, lakini baada ya hapo alipata faraja kwa kutoka sare na Manchester United na kuwashinda Fulham na Sunderland mechi zilizofuata.

 

Makocha wanaohusishwa na kuchukua mikoba ya AVB ni pamoja na kocha wa sasa wa Urusi, Fabio Capello, kocha wa zamani wa Chelsea, Roberto Di Matteo, bosi wa Swansea, Michael Laudrup na Mkurugenzi wa Ufundi wa Spurs wa sasa, Franco Baldini. Anatajwa pia kiungo wa zamani wa Spurs na kocha wa zamani wa taifa wa England, Glenn Hoddle.

 

AVB analaumiwa kwa mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na makubaliano ya kumuuza Gareth Bale, japokuwa mwenyekiti alihusika kwa kiasi kikubwa pia na kuwaletea fedha nzuri.

 

Lawama nyingine ni aina ya usajili aliofanya ambao hauoneshi tija na wala habadiliki katika kuipanga timu yake, ambapo msimu huu alileta wachezaji wanaoitwa magamba kama Paulinho, Roberto Soldado, Nacer Chadli, Etienne Capoue, Christian Eriksen, Vlad Chiriches na Erik Lamela kwa fedha nyingi. Wamefunga mabao 15 tu kati ya mechi 16 kubwa, idadi ya mabao ambayo ni ndogo kuliko aliyofunga Luis Suarez wa Liverpool mwenyewe.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version